Majina ya wabunge wa viti maalumu wapatao 112, sawa na asilimia 40 ya wabunge 264 wa majimbo yote ya Tanzania yatatajwa Novemba 5,2015 na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.Watajumuika na 10 wa kuteuliwa na Rais, watano wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Spika (ikiwa atachaguliwa kutoka nje ya wabunge) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Vyama vitatu kati ya 22 vya siasa vilivyoshiriki kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ndivyo vyenye uhakika wa kupata wabunge wa viti maalumu ambao majina yao yatatangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kesho.
Vyama vya CCM, Chadema na CUF, vinatarajiwa kupata wabunge hao kutokana na jumla ya kura za wabunge majimboni, kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 78 (1) kinachoelekeza kuwa chama kilichofikisha asilimia 5 ya kura zote halali za wabunge, ndiyo kitakachopendekeza majina ya wabunge wa viti
maalumu.
Wabunge wa viti maalumu wanaotarajiwa kupatikana ni 112, sawa na asilimia 40 ya wabunge 264 wa majimbo, ambao watajumuika na 10 wa kuteuliwa na Rais, watano wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Spika (ikiwa atachaguliwa kutoka nje ya wabunge) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge wa Chadema, John Mrema alisema jana kuwa pamoja na kuwa majimbo mengine hayajafanya uchaguzi, chama hicho kilichopata wabunge 34 hadi sasa, kinaweza kupata wabunge 52 wa viti maalumu.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya alisema wanatarajia kupata wabunge wa viti maalumu 12, licha ya kushinda majimbo 35, kwa kuwa wabunge wengi walioshinda ni wa majimbo ya upande wa Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Rajabu Luhavi alisema wamefanya majumuisho ya kura za chama hicho, wamepata asilimia 73 ya kura, hivyo wanatarajia kuwa watapata wabunge wa viti maalumu wengi kuliko vyama vingine.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima alisema wanaendelea na kazi ya uchambuzi wa fomu za wanawake zilizowasilishwa na vyama mbalimbali vya siasa, ili kuwapata wabunge wa viti maalumu ambao majina yao yatatolewa baada ya kazi hiyo kukamilishwa.
“Tangu Septemba 25, vyama vyote vya siasa vilituletea majina ya wanawake wanaotarajia kupata ubunge wa viti maalumu, tunaendelea kuchambua fomu zao ili tuhakiki sifa walizopendekezwa na vyama vyao kwa idadi inayotakiwa kabla ya kuwatangaza,” alisema Kailima.
Alisema orodha ya majina ya wagombea iliyowasilishwa kwa Tume na kila chama, ndiyo itakayotumiwa na NEC.
0 comments:
Post a Comment