Mmoja afariki kwa maradhi ya Ebola nchini Saudia
Wizara ya Afya ya Saudi Arabia imetangaza kuwa mhanga
wa kwanza wa maradhi ya Ebola amefariki dunia nchini humo. Taarifa
iliyotolewa na Wizara ya Afya ya Saudi Arabia imeeleza kuwa, watu wote
waliokutana na mhanga huyo baada ya kurejea safari ya kikazi nchini
Sierra Leone wanapasa kuwa chini ya uangalizi maalumu wa kiafya.
Wizara
ya Afya ya Saudi Arabia imeongeza kuwa, vipimo vya kimaabara
vilivyochukuliwa kwa mgonjwa huyo vilionyesha kwamba, raia huyo wa
Saudia alikumbwa na maradhi ya Ebola wakati alipokuwa nchini Sierra
Leone kikazi.
Mara baada ya kutangazwa kujitokeza maradhi ya Ebola katika
nchi za Sierra Leone, Liberia na Guinea Conakry, serikali ya Saudi
Arabia ilichukua hatua za tahadhari za kukabiliana na maradhi hayo
hatari yasiyokuwa na tiba wala chanjo, kwa kupiga marufuku utoaji viza
kwa mahujaji wa nchi hizo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO),
zaidi ya kesi 1,600 za maradhi hayo zimeripotiwa katika nchi za Sierra
Leone, Liberia na Guinea Conacry, ambapo watu zaidi ya 880 wamefariki
dunia. Shirika la WHO limeeleza dalili za ugonjwa wa Ebola kuwa ni homa
kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuuma kichwa na
vidonda kooni. Imeelezwa kuwa, mara nyingi dalili hizo hufuatiwa na
kutapika, kuharisha, vipele vya ngozi, figo na ini kushindwa kufanya
kazi na kwa baadhi ya wagonjwa hutokwa damu ndani na nje ya mwili.
Ugonjwa wa homa ya Ebola huambukiza kwa kasi na unaenea
kati ya mtu na mtu kwa kugusa damu na majimaji kutoka mwilini mwa mtu
aliyeambukizwa ugonjwa huo. Aidha imeelezwa kuwa, mtu huambukizwa
ugonjwa huo kwa kugusa maiti au mizoga ya watu au wanyama waliopatwa na
maradhi hayo.
0 comments:
Post a Comment