Rais Vladimir Putin wa Russia amemuru kuchuliwe hatua zinazohitajika za kujibu mapigo kwa vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi dhidi ya nchi hiyo. Rais wa Russia Jumanne wiki hii alisisitiza juu ya udharura wa kuwaunga mkono wazalishaji wa ndani ili kuweza kukabiliana na vikwazo vya Magharibi. 

Putin amesema kuwa serikali ya Moscow ina jukumu la kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na vikwazo vya Marekani na nchi za Ulaya dhidi ya Russia. Kwa mtazamo wa Putin, jibu la vikwazo hivyo linapaswa kuchukuliwa kwa makini na kuwalinda wazalishaji wa ndani. Ameongeza kuwa jibu hilo la vikwazo vya Magharibi dhidi ya Moscow halipasi kuwa na madhara kwa watumiaji.

Inaonekana kuwa wimbi la vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Russia na kuanza kuonekana wazi taathira zake, kumewalazimisha viongozi wa Russia kutafuta njia ya kupunguza taathira zake na wakati huo huo kutoa jibu mwafaka kwa Magharibi na waitifaki wake.

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Russia Dimitry Medvedev ameonya kuhusu vikwazo hivyo vya Marekani dhidi ya nchi yake. Medvedev amesisitiza katika kikao cha kuchunguza bajeti ya Russia ya mwaka 2015 hadi 2017 kuwa, hali ya sasa ya uchumi wa nchi hiyo ikiwa ni pamoja na taathira mbaya za vikwazo hivyo, vinapaswa kuzingatiwa ndani ya bajeti hiyo.
VladimirPutinNewYear2012-2.png
Raisi wa Urusi Viadmir Putin

Waziri Mkuu wa Russia alisema pia kuwa, kuna uwezekano serikali ya Moscow ikalazimika kuongeza kodi katika bajeti ya mwaka ujao ili iweze kufidia athari za vikwazo hivyo vya Magharibi.

Marekani na Umoja wa Ulaya mwezi uliopita ziliiwekea Russia vikwazo zaidi kufuatia kushadidi hitilafu kati ya nchi hizo na Russia. Vikwazo hivyo vimeshadidishwa zaidi baada ya kutunguliwa ndege ya Malaysia katika anga ya mkoa wa Donetsk huko mashariki mwa Ukraine Julai 17 mwaka huu. Miongoni mwa vikwazo hivyo ni vile vinavyozipiga marufuku benki muhimu za serikali ya Russia kufikia kwenye masoko ya fedha ya nchi za Magharibi.

Ikumbukwe kuwa Umoja wa Ulaya umeziwekea vikwazo benki tano nyingine za Russia zikiwemo Benki ya Kilimo na Benki ya Vensh Torg. Vikwazo hivyo vimesababisha matatizo katika soko la uwekezaji la benki za Russia. Mbali na vikwazo hivyo vya kibenki, Marekani na Umoja wa Ulaya umeiwekea Moscow vikwazo vya kuuza silaha, vikwazo dhidi ya makampuni mawili makubwa ya nishati ya Russia na vilevile vikwazo vya kuiuzia Russia zana za kuzalisha mafuta.

Ikulu ya Marekani White House hivi karibuni ilitangaza kuwa hivi sasa inashirikiana na Umoja wa Ulaya na kundi la au G-7 ili kuiadhibu zaidi Russia. Miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Marekani na waitifaki wake dhidi ya Russia ni pamoja na marufuku ya kusafiri dhidi ya viongozi wa ngazi za juu na ngazi za kati wa Russia na vilevile baadhi ya wawekezaji na wakurugenzi wa makampuni ya Kirusi kwenda Marekani na katika nchi za Ulaya na kufunga akaunti zao.

Russia kwa upande wake inasisitiza kuwa itatoa jibu kali kwa vikwazo hivyo vya Marekani na waitifaki wake. Kwa msingi huo inaonekana kuwa kwa mara ya kwanza kabisa baada ya kipindi cha Vita Baridi, dunia itashuhudia mpambano halisi na mkali wa kisiasa, kiuchumi na kijeshi baina ya nchi za Magharibi na Russia.
Imeandaliwa na Kibindo,Zanialy kwa msaada wa mtandao

0 comments:

 
Top