MBUNI ni ndege mwenye ushirikiano zaidi ya binadamu hasa katika kipindi cha kuatamia mayai mbuni hugawana majukumu ambako jike huatamia wakati wa mchana na dume huatamia wakati wa usiku.
 Kipindi cha kupandana kwa mbuni huwa ni kuanzia mwezi Machi na kuishia mwezi wa Septemba, hii hutegemeana na mazingira wanapoishi.
Mayai ya mbuni huatamiwa kwa muda wa siku 42 hadi kutotolewa vifaranga na kwa wastani mbuni hutaga mayai kati ya 40 hadi 100 kwa mwaka.
Uzito wa yai la ndege huyu ni takribani kg. 1.4 ambao ni zaidi ya mara ishirini ya uzito wa yai la kuku na ili kupika yai la mbuni hadi lichemke inachukua zaidi ya saa moja.
Kiota cha mbuni ni chatofauti na viota vya ndege wengine, huchimbwa aridhini katika shimo ambalo huwa lina kina cha sentimita 30 hadi 60 kwenda chini.
Mbuni ni ndege mkubwa kuliko wote hapa duniani ambaye hawezi kuruka licha ya kuwa na mabawa kama ndege wengine warukao.
Kwa muonekano mbuni ni ndege mkubwa mwenye shingo na miguu mirefu ambayo humufanya aonekane kuwa ndege mkubwa kuliko ndege wengine wenye sifa sawa na mbuni .
Japokuwa ndege huyu ana mabawa cha kushangaza hana uwezo wa kuruka kama ndege wengine wenye sifa sawa ambao tumezoe kuwona wakiruka angani.
 Katika mabawa ya ndege huyu kila upande huwa kuna manyoya 16 ya mwanzo,katikati huwa 4 na ya mwisho yanakuwa ni kati ya 20 hadi 23 na kwenye mkia huwa kuna manyoya yasiyopungua 50 hadi 60.



Mbuni anaweza kukimbia kwa mwendokasi ambao hufika hadi takribani km. 70 kwa saa, mwendokasi huu hupelekea mbuni kuwa na sifa ya pekee kabisa kuliko ndege wengine.
Mguu wa mbuni una vidole viwili  vyenye kucha kwa mbele na kidole cha nje huwa hakina kucha wakati ndege wengine huwa na vidole vitatu hadi vine na uwepo wa vidole hivi humsaidia kuwa na mwendo kasi wa ajabu sana kuliko ndege wengine duniani.
Mbuni akiwa katika mwendo huweza kufikia mita tatu hadi tano, mwendokasi huu huweza kumsaidia mbuni kukimbia panapotokea hatari ya kuvamiwa na adui au kuwahi kwenda kuatamia mayai kama mvua inakaribia kunyesha wakati akiwa mbali.
 Mabawa yake husaidia wakati wa kukimbia na kuhifadhi joto katika mazingira ya hali ya hewa tofauti kwasababu mbuni hupatikana katika mazingira ya hali ya hewa ya baridi na joto, kwahiyo kunapokuwa na baridi hukunja mabawa ili kuhifadhi joto na kuyapanua kuachia joto litoke wakati wa joto kali.
Mabawa ya ndege huyu hutumika kufunika vifaranga wakati wa mvua, jua kali na hata wakati wa baridi kali na anapopanua mabawa yake huweza kufikia upana wa mita mbili.
Tangu kutotolewa vifaranga huchukua takribani miaka miwili hadi minne kuwa na uwezo wa kutaga mayai au kupanda, lakini jike hutangulia kukomaa miezi sita kabla ya dume.
Katika kipindi cha mwaka wa kwanza tangu kuanguliwa mbuni huwa na uzito unaofikia kg.45 na kwa wastani mbuni aliyekomaa huwa na uzito unaoanzia kg.63 hadi kg.145.
Kulingana na utafiti uliofanywa mbuni wanaopatikana Afrika mashariki wana uzito unaofika wastani wa kg. 115 kwa dume na kg. 100 kwa jike.
Katika kipindi cha miaka miwili hadi minne mbuni dume huwa na urefu unaofikia futi sita na jike huwa na urefu unaofikia futi tano.
Urefu huu uko sawa au unazidi ule wa binadamu wa kawaida mwenye urefu wa futi tano na kinachosababisha urefu huu ni shingo na miguu ambayo hufanya kichwa kuwa juu takribani futi tano hadi tisa kutoka ardhini.
 Inaaminika kuwa ndege huyu ana macho makubwa kuzidi wanyama wote waishio ardhini, ambayo kipenyo chake hufikia mm.50, lakini kichwa cha mbuni ni kidogo sana ukilinganisha na ukubwa wa mbuni.
Miguu ya mbuni kwa kawaida haina manyoya na rangi ya manyoya ya mbuni dume yaweza kuwa nyeusi na nyeupe, huku yale ya kwenye mkia yakiwa meupe na jike huwa na rangi ya kahawia, kijivu na nyeupe.
Kichwa na shingo kwa kiasi kikubwa huwa wazi pasipokua na manyoya, huku kichwa kikiwa kipana pasipokua na kitu kilichochongoka kwa juu kama cha kuku.
Kwa kawaida mbuni huishi kwa wastani wa miaka takribani 50 hadi75 kwa mujibu wa tafiti ambazo zimefanywa na wataalam mbalimbali.
Kama ilivyo kawaida ya viumbe hai wengi kuishi kwa pamoja, mbuni nao huishi katika makundi na cha ajabu zaidi ni pale inapotokea mbuni zaidi ya moja wametaga mayai katika kiota kimoja kila mmoja huweza kutofautisha mayai yake na mengine.
Chakula kikuu cha mbuni kwa kawaida huwa ni nafaka, matunda mbalimbali, maua na wadudu jamii ya panzi. Pia ifahamike kuwa mbuni hana meno huku akiwa na uwezo wa kuishi bila kula kwa siku kadhaa.
Hii husababisha kutumia maji yaliyomo mwilini na yale yanayopatikana katika mimea yenye unyevunyevu wanayokula.
Kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wa kuishi bila kula wala kunywa, huweza kupungua uzito hadi asilimia 25 ya uzito wa mwili, lakini mbuni hupenda sana maji yanapopatikana huweza pia kuogelea.Tofauti na ndege wengine wote mbuni wana mfumo ambao hutofautisha mkojo na uchafu mwingine.
Mbuni hutembea pamoja na wanyama wengine kama Pundamilia na Swala, katika kipindi ambacho hakuna mvua mbuni hutembea katika makundi ambayo huwa yanaanzia mbuni watano hadi hamsini ambayo huwa kuna kiongozi wa kundi.Wakati wa kipindi cha baridi mbuni hutembea katika makundi au mmoja mmoja.
Manyoya ya mbuni hutumika katika biashara kwa kutengenezea bidhaa za mapambo mbalimbali, kwaajili ya kufutia vumbi na pia ngozi hutumika kutengenezea bidhaa za ngozi.Biashara ya manyoya ya mbuni imeanza tangu karine nyingi zilizopita hasa enzi za kipindi cha ustaarabu wa mwanzo  katika dola ya Misri ambayo ilikua inajihusisha na kutafuta na kuuza manyoya ya mbuni.

Wanahistoria wengi wanaamini kuwa mbuni wamekua wakiwindwa tangu maelfu ya miaka ya zamani sio kwasasbabu ya nyama tu, bali pia kwa uzuri wa manyoya unaovutia sana.
Manyoya ya mbuni yana historia ya kusisimua sana kwasababu hapo zamani katika dola ya Misri ya kale yalikua yakitumika kama alama ya haki na kwa kipindi cha sasa yamekua yakitumiwa na wataalam wa mavazi kwa ajili ya kuweka nakshi kwenye mitindo mbalimbali ya mavazi.

Haya manyoya ni ya kipekee kwasababu pamoja na uwezo wa kiteknolojia wa binadamu bado hajaweza kutengeneza manyoya yenye ubora unaofanana na yale ya mbuni.
Upatikanaji wa manyoya haya umekua ukipatikana kwa njia nyingi ikiwemo kutoa manyoya kabla ya mbuni kuchinjwa na kutoa kutoka kwa mbuni ambaye amekomaa.

Yakishatolewa ndani ya kipindi cha miezi nane manyoya mengine huwa yameshakua tena na katika nchi ambazo zinafuga mbuni kuna wapo wafugwao kwaajili ya nyama huku wengine kwa lengo la kupata manyoya.
0763955576
MWISHO

0 comments:

 
Top