Wakati sintofahamu juu ya hatima ya uchaguzi visiwani Zanzibar ikiendelea, Rais Jakaya Kikwete ameiamuru ofisi yake kusaidia kufanikisha mazungumzo baina ya mgombea wa urais wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad na Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamnyange.
Taarifa ilitolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu kwa vyombo vya habari jana, hatua hiyo ilifuata baada ya uongozi wa CUF kumuomba Rais Kikwete afanikishe mazungumzo na Mwamnyange juu ya masuala yanayoendelea visiwani humo.
Hata hivyo, undani wa mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika baina ya pande hizo mbili hayakuelezwa kwa kina.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa awali Rais Kikwete alipokea malalamiko juu ya utendaji wa baadhi ya polisi visiwani humo wakati huu wa uchaguzi na kwamba amemuagiza Mkuu wa jeshi hilo, Ernest Mangu kuchunguza madai hayo na kutoa mrejesho baada ya uchunguzi.
Kwa kipindi cha siku sita sasa Zanzibar imeingia kwenye sintofahamu na mgogoro wa kikatiba baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 na kuamua urudiwe upya.
Siku mbili zilizopita, Maalim Seif aliwaambia wanahabari kuwa baada ya uamuzi huo wa ZEC, amekuwa akifanya juhudi za kutafuta ufumbuzi kwa kukaribisha mazungumzo na viongozi wanzake wa kitaifa wakiwamo Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, lakini wamekuwa wakimpiga chenga.
Dk Shein ni mgombea wa urais wa CCM visiwani humo. Hata hivyo, Ikulu jana ilieleza kuwa madai ya Maalim Seif siyo ya kweli kuwa Rais Kikwete alikataa mazungumzo bali maombi aliyoyapelekewa kutoka CUF ni malalamiko juu ya vitendo vya polisi na kuomba mazungumzo na Mwamunyange.
Taarifa hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu,Salva Rweyemamu ilisema Rais anaguswa na hali ya kisiasa na kiusalama inayoendelea visiwani humo kama walivyo Watanzania wengine.
MWANANCHI
Wabunge wote wateule, wametakiwa kufika Ofisi Ndogo ya Bunge Dar es Salaam, ili kushiriki hafla ya kuapishwa kwa Rais mteule, Dk John Magufuli.
Wabunge hao kutoka majimbo 259 nchini walichaguliwa katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumapili ya Oktoba 25, ambao pia ulimpa ushindi Dk John Magufuli wa CCM, dhidi ya mshindani wake wa karibu Edward Lowassa wa Chadema aliyeungwa mkono na Ukawa.
Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema wabunge hao wateule wanatakiwa kuwasili kwenye ofisi hizo akiwa na cheti kinachoonyesha kateuliwa kuwa mbunge, kilichotolewa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo husika.
“Cheti hicho, kitawasilishwa kwa maofisa wa Bunge wakati wa zoezi la usajili, pia kila mbunge mteule atatakiwa kubeba kitambulisho kingine chochote kilichotolewa na mamlaka inayotambulika, kinachoonyesha jina lake kamili kama lilivyoandikwa kwenye cheti cha ubunge,”Joel.
Ameongeza: “Uchaguzi umekwisha, lakini baadhi ya majimbo bado kutokana na sababu mbalimbali. Masikio ya wananchi na wabunge wateule ni kujua nini kitafuata upande wa ofisi ya Bunge, ndiyo maana leo (jana ), tunatangaza kuwaita wateule wote kufika Dar es Salaam Novemba 4 mwaka huu.”
Amefafanua kwamba usajili kwa wabunge wote wateule utafanyika viwanja vya Bunge Mjini Dodoma na kila mbunge atajitegemea usafiri kwa ajili ya shughuli hiyo itakayofanyika kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 11.
Kuhusu kuongezeka kwa majimbo, Joel alisema wamejipanga na kuongeza viti ili kuhakikisha wabunge wote wanapata nafasi ya kuketi kwenye ukumbi huo. “Hatujabadilisha ukumbi bali tumeongeza idadi ya viti kwa kazi mbili maalumu .
Moja ni kwa ajili Rais atakapozindua Bunge na pili kwa wabunge wote wakiwamo wa viti maalumu, ambao bado hatujua idadi yao,” alisema Joel.
Kwa mujibu wa Joel, mkutano huo wa kwanza unatarajiwa kuanza siku ambayo Rais ataitisha Bunge na utahusisha uchaguzi na kiapo kwa Spika, viapo kwa wabunge wote wateule, kuthibitisha jina la Waziri Mkuu, uchaguzi wa Naibu Spika na ufunguzi rasmi wa Bunge la 11.
Joel alitumia nafasi hiyo kuvikumbusha vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu vilivyo na nia ya kusimamisha mgombea uspika kuanza mchakato mapema kwenye ngazi ya vyama, kabla ya tangazo la nafasi ya Spika kuwa wazi.
Amesema lengo la kuvikumbusha ni kuvitaka vikamilishe mchakato kwa wakati na kuwasilisha jina la mgombea kwa Katibu wa Bunge.
NIPASHE
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi, David Kafulila, ambaye ametangazwa kushindwa katika jimbo hilo uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu, ameibuka na kusema anakusudia kwenda mahakamani ili atangazwe kuwa mshindi wa jimbo hilo.
Amedai kwa mujibu wa kura alizokusanya kupitia mawakala wake katika vituo 182, alishinda kwa kura 34,149 dhidi ya mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Husna Mwilima, aliyepata kura 32,982, lakini tume ikamtangaza kuwa mshindi.
Kafulila alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na uchaguzi huo, akidai ameporwa ushindi wake na nguvu ya dola imetumika kuhakikisha anakosa ushindi huo.
“Ninachofahamu mimi ni Mbunge wa Kigoma Kusini, ila nilihujumiwa na watumishi wa tume kwa kubadili matokeo yangu na kumtangaza mgombea wa CCM kuwa ni mshindi, hivyo nitaenda Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kudai haki yangu na kutangazwa mshindi,” Kafulila.
Alisema atakachokifuata mahakamani siyo kurudiwa kwa uchaguzi bali kuiomba mahakama kumtangaza mshindi kwani ana vielelezo vyote.
“Wiki ijayo nitakuwa nimekamilisha mipango ya kwenda mahakamani, nina fomu zote 382 kutoka katika kila kata, vituo 182 vilivyotumika kupiga kura zinazoonyesha idadi ya kura zangu. Nina imani mahakama haitatumia mlolongo mrefu kutoa hukumu kwa sababu nina vielelezo vya kutosha,” Kafulila.
Aliwataka wananchi wa jimbo hilo kutokata tamaa na taarifa za kukosa ubunge wake na kuwataka kuwa wavumilivu wakati wakisubiri maamuzi ya mahakama.
Kafulila alipoulizwa sababu anayodhani kumkosesha jimbo hilo au kuibiwa ushindi kama alivyodai, alisema kutokana na kazi kubwa aliyoifanya Bunge lililopita ya kuibua masuala ya ufisadi ikiwamo sakata la Tegeta Escrow.
Alidai kudhibitisha kuwa njama zilitumika, aliwekewa ulinzi mkali wa dola wakati wa upigaji kura na kipindi cha kusubiri matokeo.
“Nguvu ya dola ilitumika sana ili kuhakikisha Kafulila ninashindwa, polisi walikuwa ni wengi sana pia matokeo yalichelewa kutangazwa isivyo kawaida,” alisema.
Kafulila alisema alishangazwa na kitendo cha mawakala wa tume kuahirisha kazi ya ujumuishaji wa kura mara kwa mara licha ya sheria ya uchaguzi kutoruhusu.
“Kazi ya ujumuishaji ilikuwa ikiahirishwa mara mbili na wakati mwingine kuchukua zaidi ya saa 7 na saa 10 hali ambayo siyo ya kawaida,” alidai Kafulila.
Akizungumzia hatma yake juu ya kupiga vita ufisadi, Kafulila alisema ataendelea na harakati hizo.
Alisema kwa sasa anaandaa vitabu vinavyozungumzia ufisadi kikiwamo kinachoitwa‘Escrow Unfinished Business’, ambacho kinaelezea vizuri masuala hayo ambayo amekuwa akiyapiga vita.
NIPASHE
Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, amesema hata kama vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) vimefanikiwa kumwangusha kwenye kinyang’anyiro cha ubunge katika Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, bado ana nguvu ya kuendelea kuwania nafasi mbalimbali za kisiasa na wala hajakata tamaa ya kukisuka upya chama chake.
Mrema aliangushwa katika kiti hicho na hasimu wake kisiasa, James Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi, aliyevunja rekodi ya kupata kura nyingi kwa upande wa wabunge wa upinzani, baada ya kuibuka na ushindi mnono wa kura 60,187 dhidi ya 6,416 alizoambulia Mrema (TLP) aliyekuwa akishikilia jimbo hilo huku mgombea wa CCM, Innocent Shirima, akipata kura 16,097.
Alikuwa akihojiwa jana na kituo kimoja cha redio mkoani Kilimanjaro kuhusu majaliwa yake kisiasa, baada ya yeye na chama chake kukosa uwakilishi kwenye Bunge na Halmashauri za Wilaya. Mbali ya kupoteza kiti cha ubunge, TLP haikuambulia hata kiti kimoja cha udiwani.
“Chama changu hakifi na wala sijakata tamaa, tutaanza moja na ninawaomba wanachama wa TLP watulie…Nitashirikiana na Rais ajaye aliyetangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), na tutakijenga chama chetu…Hata Dk. John Magufuli, anajua mimi ni mchapakazi na alinipigia debe na wananchi wakapuuza,” alisema Mrema.
Katika Mkoa wa Kilimanjaro wenye majimbo tisa ya uchaguzi, viti saba vya ubunge vimenyakuliwa na baadhi ya vyama vinavyounda Ukawa vya Chadema na NCCR-Mageuzi, huku majimbo mawili ya Mwanga na Same Magharibi, yakiangukia CCM.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, Chadema iliyovuna wabunge sita na NCCR-Mageuzi yenye mbunge moja mkoani Kilimanjaro, sasa zitaunda halmashauri tano za wilaya ambazo ni Moshi Mjini, Hai, Siha, Rombo, Moshi Vijijini na Vunjo; wakati CCM ikiwa imeambulia Halmashauri mbili za Mwanga na Same.
Majimbo hayo na idadi ya kata ambazo Chadema na NCCR-Mageuzi zitaunda halmashauri zake ni kama ifuatavyo;
Moshi Mjini, Chadema imeshinda Kata 19 kati ya 21 na CCM imepata Kata mbili za Bondeni na Kilimanjaro, wakati Jimbo la Hai, Chadema imeshinda kata 16 kati ya 17, ambapo Kata moja ya Bomang’ombe ndio pekee haijafanya uchaguzi kutokana na mgombea wa CCM kufariki dunia wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.
Aidha, Chadema iliyoshinda kata 27 kati ya 28 za Wilaya ya Rombo, ndiyo itakayounda halmashauri ya wilaya hiyo, huku NCCR-Mageuzi iliyoshinda kata nane, kati ya 16 na Chadema iliyoshinda viti 15 vya udiwani katika Jimbo la Moshi Vijijini, sasa zitaunda Halmashauri moja ya Wilaya ya Moshi.
NIPASHE
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba,amejitokeza kwa mara ya kwanza kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam na kumtaka Rais Jakaya Kikwete amalize haraka mgogoro wa uchaguzi uliopo Zanzibar kabla ya kumpisha mrithi wake, Dk. John Magufuli.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi kuu za CUF jana, Lipumba alisema jaribio lolote la kutaka Rais Kikwete aondoke na kumuachia Magufuli suala hilo ni sawa na kumtwisha rais ajaye (Magufuli) mzigo mkubwa ambao hatauweza na mwishowe ni kusababisha madhara makubwa visiwani humo ikiwamo vurugu na uvunjifu wa amani.
Profesa Lipumba aliyasema hayo ikiwa imepita takriban miezi mitatu tu tangu atangaze kujiuzulu uenyekiti wa CUF Agosti 6, 2015 ili awe mwanachama wa kawaida wa chama hicho.
Lipumba alitangaza kuchukua uamuzi huo wa utata kutokana na kile alichodai kuwa ni kupinga uamuzi wa chama chake na vingine vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwapokea waliokuwa makada wa CCM na kuwapa nafasi ya kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015.
Akieleza zaidi jana, Lipumba alisema Kikwete ana uelewa mpana wa masuala ya kisiasa na kwamba akiamua kwa dhati, anao uwezo mkubwa wa kumaliza mgogoro uliopo sasa Zanzibar kabla ya kumkabidhi madaraka Magufuli ifikapo Ahamisi ya Novemba 5 mwaka huu.
Alisema Rais Kikwete amewahi kuishi Zanzibar alipokuwa wakati katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na anaijua hali ya kisiasa visiwani humo kuliko ilivyo kwa mrithi wake, Dk. Magufuli.
“ Suala hili Rais Kikwete ulimalize kabla ya Dk. Magufuli kuapishwa… usimwachie kwa kuwa (ni wazi) utampa mzigo mkubwa ambao hatauweza na (hakika) nchi itavurugika,” alisema Lipumba.
Hivi sasa, Zanzibar imeingia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kutangaza kufutwa kwa uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 kutokana na kile alichodai kuwa ‘haukuwa huru na wa haki’, ingawa ndiyo uliotumika kupata kura zilizompa ushindi Magufuli kuwa Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
huo wa Jecha umepingwa na CUF ambayo mgombea wake, Maalim Seif Sharif Hamad, aliitisha mkutano na waandishi wa habari hapo kabla na kuwaonyesha karatasi za matokeo halisi ya kura kutoka katika vituo vyote visiwani humo zkionyesha kuwa ameshinda kwa asilimia 52.87.
Akielezea zaidi kuhusiana na hali ya Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu, Lipumba alisema njia pekee ya Rais Kikwete kumaliza mgogoro huo ni kuitaka ZEC iendelee na mchakato wa majumuisho ya kura na kumtangaza mshindi ambaye ni wazi anajulikana kuwa ni Maalim Seif, hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa karatasi za matokeo ya kura zilizokusanywa kutoka kwenye vituo vyote visiwani humo.
Alisisitiza kuwa endapo Rais Kikwete atamkabidhi madaraka Magufuli kabla ya kumaliza mgogoro uliopo Zanzibar, ni dhahiri atakuwa amemuweka kwenye wakati mgumu na upo uwezekano kuwa mrithi wake huyo atatumia nguvu kubwa kutatua mgogoro huo, jambo ambalo ni la hatari zaidi kwa hatma ya Zanzibar na taifa. Aliongeza kuwa Dk. Magufuli hataweza kuiongoza nchi kwa amani ikiwa Zanzibar kutakuwa na machafuko, hivyo Rais Kikwete anapaswa kulimaliza jambo hilo kabla hajamaliza muda wake wa uongozi.
“Kama watu wanavyomuita Magufuli kuwa ni tingatinga au bulldozer, basi ni dhahiri atatumia nguvu katika kutatua mgogoro huo… na jambo hilo litakuwa ni la hatari kubwa kwa Zanzibar na taifa,” alisema Lipumba.
NIPASHE
Wakati saa 48 zilizotolewa na mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF),Maalim Seif Shariff Hamad kutaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuendelea na mchakato wa majumuisho ya kura na kumtangaza mshindi wa urais wa Zanzibar zikiwa zimemalizika, Ikulu ya Jamhuri ya Muungano imesema haijapokea maombi ya Maalim Seif kutaka kuonana na Rais Jakaya Kikwete.
Ijumaa iliyopita, Maalim Seif aliwaambia waandishi wa habari visiwani Zanzibar kuwa baada ya ZEC kufuta uchaguzi Jumanne iliyopita, alifanya jitihada kadhaa za kuwasiliana na Rais Kikwete na pia Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ili kuzungumzia suala hilo kwa maslahi ya Zanzibar lakini wito wake huo umekuwa ukipuuzwa.
Maalim Seif alisema tangu kufutwa kwa uchaguzi, amefanya juhudi za kutafuta ufumbuzi kwa kukaribisha mazungumzo na viongozi wenzake wa kitaifa akiwamo Rais Kikwete na pia Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, lakini wote wamekuwa wakimkwepa, licha ya kuanza kuwatafuta kwa kutumia mawasiliano ya simu na ujumbe kupitia wasaidizi wao, akitaka wakutane.
Hata hivyo, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, ilieleza kuwa Ikulu imesikitishwa na madai ya Maalim Seif, ikieleza kuwa siyo kweli.
Badala yake, Ikulu imesema haijapokea ombi lolote kutoka kwa Maalim Seif la kutaka kukutana na Rais Kikwete tangu siku ya kupiga kura na hata baada ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kufuta uchaguzi wa Zanzibar.
Taarifa hiyo ya Ikulu imesema kile ambacho Rais Kikwete amekipokea ni malalamiko ya CUF kuhusu baadhi ya vitendo kutoka kwa baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi Zanzibar na ombi kwa ajili ya kuwezesha mazungumzo kati ya Maalim Seif na Mkuu wa Majeshi (CDF), Jenerali Davis Mwamunyange.
“Baada ya hapo, Rais Kikwete, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, kuchunguza madai haya ya CUF na kumletea taarifa. Kadhalika, ametoa maelekezo ofisini kwake ya kuwezesha mazungumzo kati ya Jenerali Mwamunyange na maafisa wa CUF,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa Ikulu Rais Kikwete amekuwa akiguswa na hali ya kisiasa na usalama wa Zanzibar kama ilivyo kwa Watanzania wengine na amekuwa akifanya kazi bila kuchoka huku akipata ushauri wa kina juu ya kilichotokea Zanzibar siku chache zilizopita na kupata ufumbuzi.
HABARILEO
Watahiniwa 448,358 wa shule na wa kujitegemea wanatarajia kufanya mtihani wa kumaliza Kidato cha Nne unaotarajia kuanza kufanyika leo nchi nzima.
Idadi hiyo ya watahiniwa ni ongezeko la watahiniwa 150,870 ukilinganisha na watahiniwa 297,488 waliosajiliwa mwaka 2014.
Kwa mujibu wa ratiba ya mtihani huo utakaofikia tamati Novemba 27, leo watahiniwa wataanza kufanya mtihani wa Kiswahili na Civics, na watafuatiwa na kufanya Basic Mathematics na Kiingereza na keshokutwa watafanya Biolojia na Historia, na kishaJiografia na Kemia, Ijumaa Biolojia (Vitendo) na Book Keeping.
Juzi Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk Charles Msonde alisema kati ya watahiniwa hao, 394,243 kati ya 448,858 waliosajiliwa kufanya mtihani wao ni watahiniwa wa shule na wanafunzi 54,115 ni wa kujitegemea. Msonde alisema kati ya watahiniwa wa shule 394,243 waliosajiliwa, wavulana ni 193,082 ambayo ni asilimia 48.97 na wasichana 201,161 ambao ni asilimia 51.03.
“Watahiniwa 67 kati ya hao ni wasioona na watahiniwa wenye uoni hafifu ni 278 ambao maandishi ya karatasi zao za mtihani hukuzwa,” alisema Msonde.
Msonde alisema watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa kufanya mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2015 wanaume ni 26,051 sawa na asilimia 48.14 na wasichana ni 28,064 sawa na asilimia 51.86, huku watahiniwa wa kujitegemea wasioona ni wawili ambao wote ni wanaume.
Kwa upande wa Mtihani wa Maarifa (QT), Msonde alisema watahiniwa 19,547 wamesajiliwa kufanya mtihani mwaka 2015, wanaume wakiwa ni 7,225 ambayo ni asilimia 26,96 na wanawake ni 12,322 ambao ni asilimia 63.03. Mwaka 2014 walikuwa watahiniwa 14,723.
“Maandalizi yote kwa ajili ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa mtihani, vitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo katika mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani,” alisema.
Alizitaka Kamati za Mtihani za Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa na taratibu zote za mtihani zinazingatiwa ipasavyo, mazingira ya vituo yapo salama, tulivu na kuzuia mianya inayoweza kusababisha udanganyifu.
Aidha, Msonde aliwaasa wasimamizi kujiepusha na vitendo vya udanganyifu na kusisitiza kuwa Baraza litachukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kukiuka taratibu za uendeshaji wa mtihani.
HABARILEO
Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale- Mwiru amesema atazungumzia mchakato wa Uchaguzi Mkuu baadaye baada ya kukusanya taarifa za kutosha.
Akizungumza kwa njia ya simu baada ya kuombwa kutoa maoni yake kuhusu Uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni na Dk John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutangazwa mshindi, Kingunge bila kufafanua zaidi alisema: “Nitazungumzia mchakato wa uchaguzi baadaye baada ya kukamilisha kukusanya taarifa.”
Mwanzoni mwa Oktoba, Kingunge ambaye amekuwa kada wa CCM kwa miaka 61 (tangu enzi za TANU), alitangaza kujitoa katika chama hicho akisema hawezi kuendelea kuwa ndani ya chama kinachoendeshwa kwa maslahi binafsi.
Kingunge ambaye amefanya kazi kwa karibu ndani ya CCM na Serikali na marais wa wote wa awamu nne, alidai chama hicho kimepoteza mwelekeo na hakijadili mambo muhimu kama ilivyokuwa zamani.
Pamoja na Kingunge kudai hajiungi na chama kingine chochote cha siasa, alionekana kwenye jukwaa la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakati wa kumnadi mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho aliyeungwa na vyama vinavyounda Ukawa, Edward Lowassa.
Uchaguzi Mkuu ulifanyika Oktoba 25, mwaka huu, na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilimtangaza Dk John Magufuli kuwa mshindi baada ya kupata kura 8,882,935 (asilimia 58.46) na kufuatiwa na Lowassa kura 6,072,848 (asilimia 39.97).
HABARILEO
Uchaguzi wa ubunge kwa majimbo ya Handeni na Arusha Mjini umepangwa kufanyika Desemba 12, mwaka huu.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Ramadhanialisema hivi karibuni watatangaza kuanza kwa kampeni baada ya kupitisha majina ya wagombea.
Tayari, CCM imemchagua Omari Kigoda kugombea jimbo hilo baada ya kuwashinda wagombe wengine 11 ndani ya chama hicho kwa kupata kura 296 kati ya kura 666 za wajumbe.
Ramadhani alisema katika majimbo ya Lushoto na Ulanga Mashariki ambayo uchaguzi wake utafanyika Novemba 22, mwaka huu kampeni zake zimeshaanza.
Alisema kwa upande wa majimbo ya Ludewa na Masasi Mjini taratibu zake zitatangazwa baadaye. Tume ilisitisha uchaguzi wa ngazi ya ubunge katika majimbo sita kutokana na vifo vya baadhi ya wagombea katika majimbo hayo.
Mgombea wa kwanza kufariki dunia alikuwa wa Chadema Jimbo la Lushoto, Mohammed Mtoi aliyefariki dunia kwa ajali ya gari Septemba 13, alifuatiwa na aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na mgombea Jimbo la Ulanga Mashariki, Celina Kombani wa CCM aliyefariki katika Hospitali ya Apollo, New Delhi, India kutokana na ugonjwa wa saratani ya kongosho, Septemba 24, mwaka huu.
Wa tatu alikuwa Estomiah Mallah wa ACT Wazalendo Jimbo la Arusha Mjini aliyefariki dunia Oktoba 8, kwa ajali ya gari, kufuatiwa na Dk Abdallah Kigoda wa CCM Jimbo la Handeni Mjini ambaye pia alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara aliyefariki dunia Oktoba 12, akiwa katika matibabu kwenye Hospitali ya Apollo, New Delhi nchini India.
Mgombea wa tano kufariki dunia ni mgombea wa Masasi Mjini kwa tiketi ya National League for Democracy (NLD), Dk Emmanuel Makaidi Oktoba 15 baada ya kuugua ugonjwa wa kiharusi na kufuatiwa na mgombea wa Jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe aliyefariki kwa ajali ya helikopta Oktoba 16.
0 comments:
Post a Comment