Watahiniwa 448,358 wa shule na wa kujitegemea wanaendelea na  mitihani wa kumaliza Kidato cha Nne ulioanza tarehe 2 mwezi huu.
Idadi hiyo ya watahiniwa ni ongezeko la watahiniwa 150,870 ukilinganisha na watahiniwa 297,488 waliosajiliwa mwaka 2014.
Kwa mujibu wa ratiba ya mtihani huo utakaofikia tamati Novemba 27, watahiniwa wataanza kufanya mtihani wa Kiswahili na Civics, na watafuatiwa na kufanya Hisabati na Kiingereza na keshokutwa watafanya Biolojia na Historia, na kishaJiografia na Kemia, Ijumaa Biolojia (Vitendo) na Book Keeping.
Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk Charles Msonde alisema kati ya watahiniwa hao, 394,243 kati ya 448,858 waliosajiliwa kufanya mtihani wao ni watahiniwa wa shule na wanafunzi 54,115 ni wa kujitegemea. Msonde alisema kati ya watahiniwa wa shule 394,243 waliosajiliwa, wavulana ni 193,082 ambayo ni asilimia 48.97 na wasichana 201,161 ambao ni asilimia 51.03.
“Watahiniwa 67 kati ya hao ni wasioona na watahiniwa wenye uoni hafifu ni 278 ambao maandishi ya karatasi zao za mtihani hukuzwa,” alisema Msonde.
Msonde alisema watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa kufanya mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2015 wanaume ni 26,051 sawa na asilimia 48.14 na wasichana ni 28,064 sawa na asilimia 51.86, huku watahiniwa wa kujitegemea wasioona ni wawili ambao wote ni wanaume.
Kwa upande wa Mtihani wa Maarifa (QT), Msonde alisema watahiniwa 19,547 wamesajiliwa kufanya mtihani mwaka 2015, wanaume wakiwa ni 7,225 ambayo ni asilimia 26,96 na wanawake ni 12,322 ambao ni asilimia 63.03. Mwaka 2014 walikuwa watahiniwa 14,723.
Aidha Kamati za Mtihani za Mikoa na Wilaya  zinatakiwa kuhakikisha  taratibu zote za mtihani zinazingatiwa ipasavyo, mazingira ya vituo yapo salama, tulivu na kuzuia mianya inayoweza kusababisha udanganyifu.
Aidha, Msonde aliwaasa wasimamizi kujiepusha na vitendo vya udanganyifu na kusisitiza kuwa Baraza litachukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kukiuka taratibu za uendeshaji wa mtihani.

0 comments:

 
Top