Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad mapema leo ametoa wito kwa wafuasi wake kuendelea kuwa wavumilivu na kuruhusu mazungumzo yaendelee kuhusu njia bora ya kutatua mkwamo wa kisiasa visiwani Zanzibar.

Awali Maalim Seif ambaye aligombea urais wa visiwa hivyo kwa tiketi ya CUF alikuwa ametishia kuongoza maandamano ya wananchi endapo matokeo ya uchaguzi wa rais hayangetangazwa kufikia leo Jumatatu. 


Akizungumza na waandishi wa habari, kiongozi huyo wa CUF amesema jamii ya kimataifa inajitahidi kuwasaidia Wazanzibari kufikia mapatano yatakayodhamini amani na usalama na hivyo amewataka wafuasi wake waendelee kuwa watulivu.

Rais anayeondoka wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema juhudi kubwa zinafanyika ili kutatua tatizo la Zanzibar.

Siku kadhaa zilizopita, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilitangaza kufuta matokeo yote ya uchaguzi visiwani humo kutokana na kile kinachotajwa kuwa kasoro nyingi kwenye zoezi la upigaji kura la Oktoba 25. Tangazo la ZEC limepelekea kutanda hali ya wasiwasi na taharuki visiwani Zanzibar huku CUF ikishikilia kuwa ilishinda uchaguzi huo

0 comments:

 
Top