Spika wa Bunge Anne Makinda
ametangaza rasmi kutogombea tena nafasi hiyo, huku akisema kulikuwa na
wabunge watundu wanane waliomchangamsha na kumlazimisha ajifunze kwa haraka
baadhi vifungu vya kanuni za Bunge.
Makinda amekuwa mbunge tangu mwaka
1975 na alikuwa Spika kwa kipindi cha miaka mitano, wakati Samuel Sitta akiwa
Spika yeye (Makinda) alikuwa naibu wake.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana kwenye ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam, alisema atawakumbuka wabunge
hao waliomchangamsha kwenye Bunge la 10, kwa kuibua hoja za nguvu.
Aliwataja wabunge hao kuwa ni
Halima Mdee, Tundu Lissu, Ezekiah Wenje, John Mnyika wote wa Chadema, Ester
Bulaya (wakati huo alikuwa CCM), Felix Mkosamali na Moses Machali wote waliwa
NCCR-Mageuzi na Deo Filikunjombe wa CCM (kwa sasa ni marehemu).
“Nitawakumbuka sana rafiki zangu,
walikuwa wachangamfu kiasi cha kufanya nizijue kanuni kwa nguvu, mara ya
kwanza kuanza kazi nilishituka, lakini baadaye nikajifunza kumbe hivi ndivyo
ilivyo, kwa kweli lilikuwa bunge zuri,” alisema.
Alidai kusikitishwa na baadhi ya
wabunge kushindwa kwenye majimbo yao akiwamo Wenje katika Jimbo la Nyamagana
na kumsihi asikate tamaa badala yake ajipange kwa wakati mwingine.
Makinda alisema fujo za baadhi ya
wabunge zililifanya Bunge aliloliongoza kuwa na mvuto wa aina yake, kwa madai
kuwa likipoa haliwezi kuleta maana ya kuwapo kwa chombo hicho.
Alikiri kujifunza mambo mengi kwenye
Bunge aliloliongoza kutokana na kuwapo kwa wabunge wengine vijana
“Kuna mabunge ya nchi nyingine ambayo
tumeshuhudia watu wakitwangana, Bunge halitakiwi kupoa lazima wawepo watundu
wa kulichangamsha, vinginevyo litalala na kukosa mvuto,”alisema Makinda.
Alisema jambo alilojifunza kwenye
Bunge hilo, ni kutokuwa na hasira, kuwa mvumilivu, huku akijitahidi kupokea
hoja za wabunge wote bila kubagua wala kuwapo upendeleo kwa wabunge wa chama
chake (CCM).
Makinda alisema ubunge ni
uwakilishi wa wananchi na kwamba, baadhi ya wabunge ambao hawakufanya kazi
zao ipasavyo kwenye Bunge lililoisha, walichangia kukwamisha kura za chama
chake.
Aliwataka wabunge kuwatumikia
wananchi waliowachagua kwenye majimbo yao badala ya kutumia muda mwingi,
kutengeneza hoja za uongo bungeni.
Makinda (pichani) ambaye alikuwa
mbunge wa jimbo la Njombe Kusini (CCM), alisema amelazimika kustaafu nafasi
hiyo ili awaachie wengine waongoze, baada ya kuwapo bungeni kwa miaka 40.
Maisha yangu yote nimekuwa
mwanasiasa, nimeshakuwa kiongozi wa nafasi zote bungeni kwa hivyo nimeamua
kustaafu uongozi, nafikiri ni jambo zuri kuachia wengine waendelee kuongoza,”
alisema.
Alisema Spika anayetakiwa ni
lazima akubali kujifunza tabia za wabunge wake na kuwa na uwezo wa
kukabiliana na hali halisi ya bungeni.
Alisema ni lazima spika huyo awe
mvumilivu na asiwe mwepesi wa hasira badala yake atumie muda wake kujifunza
kanuni za Bunge na kuwa mwepesi wa kupokea hoja za wabunge bila kubagua ili
azifanyie kazi.
Akubali kuwa rafiki wa wabunge
wote ili baada ya Bunge, maisha mengine yaendelee. Nilikuwa rafiki wa wabunge
wote na sikuwa mwepesi wa kukasirika,” alisema.
Wakati Makinda akisema hayo, Mjini
Dodoma, baadhi ya wabunge wateule wamesema Spika wa Bunge la 11 anatakiwa
kuwa mtu mwenye hekima, uvumilivu na mwenye kuhimili mikiki mikiki ya wabunge
ambao wengi wao ni vijana na wapya.
Mbunge wa Buyungu (Chadema),
Kasuku Bilago alisema Spika anayetakiwa ni mtu makini na mwenye kuhimili
mikiki mikiki ya wabunge hao. “Siyo shughuli ndogo katika Bunge hili. Spika
anayekuja anatakiwa kuepuka upande,” alisema Bilago.
Daniel Mtaka wa Manyoni Mashariki-
(CCM), alisema: “Spika aendane na wakati. Tunahitaji asiwe mtu wa kukariri,
achukue mawazo mazuri ya kujenga nchi hata kama yanatoka kwenye upinzani.”
Mbunge wa Konde (CUF), Khatibu
Said Haji alisema Spika anayetakiwa ni yule atakayetoa uhuru wa wabunge
kuisimamia Serikali na kutozima hoja za wabunge.
Kampeni za uspika zilikuwa zikiendelea jana
katika Viwanja vya Bunge, huku baadhi ya wabunge wateule wanaomuunga mkono
Naibu Spika wa Bunge la 10, Job Ndugai wakitafuta kura kutoka kwa wabunge
wenzao wa CCM.
Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone
Lusinde alisema kampeni za kumpata spika na naibu wake ndani ya CCM
zimeshamalizika, kutokana na wabunge wengi kumuunga mkono Ndugai ambaye ni
mbunge mteule wa Kongwa, .
Kwa upande wa naibu spika
wanayemtaka ni Mbunge mteule wa Ilala, Azan Zungu ambaye alikuwa Mwenyekiti
wa Bunge katika Bunge la 10.
Zungu jana alikuwa mwanachama wa
kwanza wa CCM kuchukua fomu akiwania nafasi ya naibu spika, tofauti na
matarajio ya wengi kuwa angewania uspika.
Alisema asingetaka uspika kwa sasa,
kwani bado anaendelea kujifunza uongozi wa chombo hicho na sehemu sahihi kwa
sasa ni nafasi ya unaibu spika.
Mbunge mteule wa Kasulu Mjini,
Daniel Nsanzugwanko, jana alikuwa kada wa CCM wa 23 kuchukua fomu kuwania
uspika.
Capt: Aliyekuwa spika wa bunge Anne Makinda
Akizungumza wakati wa kurudisha
fomu Nsanzugwanko alisema amejitokeza kuwania nafasi hiyo kuliwezesha Bunge
kuisaidia Serikali ya awamu ya tano iweze kukidhi kiu ya Watanzania.
Mbali na usajili wa Bunge, maofisa
kutoka benki za CRDB na NMB walikuwa wakitoa huduma kwenye viwanja hivyo
zikiwamo za mikopo katika mahema kadhaa yaliyofungwa hapo.
Kwa upande wa mavazi, wabunge
wengi walionekana kutomudu mavazi yanayohitajika katika kupiga picha.
Mimi imenibidi kurudi nyumbani
kuvaa koti maana wamesema siwezi kupiga picha bila kuvaa koti,” alisema mmoja
wa wabunge kutoka kanda ya kusini. Mavazi mafupi yalionekana kutawala kwa
wabunge wengi wa kike vijana katika viwanja hivyo.
|
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment