Aliyekuwa mgombea wa urais wa Chadema, Edward
Lowassa anatarajia kuhutubia mkutano wa kumnadi mgombea wa ubunge wa Jimbo la
Arusha Mjini, Godbless Lema na kuwashukuru Watanzania kwa kura walizompa katika
Uchaguzi Mkuu uliopita.
Jeshi la Polisi limeridhia mkutano huo utakaofanyika
viwanja vya Shule ya Msingi Ngarenaro, lakini limepiga marufuku maandamano
yoyote.
Huu utakuwa mkutano wa kwanza wa hadhara kwa Lowassa
tangu matokeo ya uchaguzi mkuu yalipotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), ambayo yalimpa ushindi mgombea wa CCM, Dk John Magufuli. Lowassa alipata
kura 6,072,848, sawa na asilimia 39.97 wakati mshindi Dk Magufuli alijikusanyia
kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46
“Tunatarajia kesho
(leo) aliyekuwa mgombea wa urais wa Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa, Edward
Lowassa atahutubia mkutano wa kampeni wa kawaida akiongozana na viongozi
wengine wa kitaifa,” alisema Katibu wa Chadema Wilaya ya Arusha, Lewis Kopwe,
alipozungumzia kukamilika kwa maandalizi yote ya mkutano huo jana.
Kopwe alisema mkutano huo ni sehemu ya mikutano ya
kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arusha Mjini na amehimiza amani na
utulivu vitamalaki katika mkutano huo.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas,
akizungumza na Mwananchi jana alisema wamepiga marufuku maandamano ya aina
yoyote katika mikutano ya kampeni inayoendelea.
Alionya Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua
mtu yeyote ambaye ataandamana na kusababisha kuvunjika kwa amani katika Jiji la
Arusha. “Kuna watu, kwa maslahi yao, wanataka kutuvunjia amani, sasa tunaonya
tutachukua hatua kali kwa yeyote ambaye atavunja sharia,” alisema Kamanda Sabas.
Pamoja na onyo hilo, alisema kuwa hadi jana jeshi
hilo, lilikuwa halijapata barua yoyote ya kutaka maandamano na hata ikiwapo
hawatakuwa tayari kuruhusu yafanyike. Pia, alisema jeshi hilo liko vizuri na
limejipanga kuhakikisha amani na utulivu vinadumu kama ilivyokuwa wakati wa
Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 mwaka huu.
Magari ya kuwasha
Katika hali inayoonyesha kwamba Jeshi la Polisi
halitanii, jana jiji la Arusha lilikumbwa na taharuki kutokana na magari makubwa
ya kurusha maji ya kuwashwa kupitishwa mitaani huku yakiwa kwenye mwendo kasi.
Lema, ambaye anajiandaa kutetea kiti hicho alisema kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni kwamba Lowassa atazungumza leo na Watanzania, pia kuwashukuru kwa kumpigia kura nyingi
Naye Mbunge mteule wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi
“Sugu” alisema katika mkutano huo Chadema watatoa tamko zito la kwanza mara
baada ya uchaguzi huo wa madiwani, wabunge na rais kumalizika
0 comments:
Post a Comment