MAONI YA WADAU WA ELIMU YATHAMINIWE
Na Kibindo,Zanialy

LICHA ya hatua tuliyopiga  kwenye sekta ya elimu tangu uhuru wa nchi yetu mwaka 1961ikiwemo ongezeko la shule pamoja na vyuo vya elimu, bado sekta hii nyeti inakabiliwa na changamo nyingi hali inayosababisha kudhoofu kwa hali ya elimu nchini.
Kwa kutambua umuhimu wa sekta hii nyeti ya elimu wadau wa elimu wanafanya jitihada mbalimbali   kuinusuru sekta hii ,makala hii inatazama moja ya kongamano lililoandaliwa na shirika la HakiElimu kwa kushirikiana na Umoja wa walimu wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSTA).
Kongamano hilo lilifanyika mnamo tarehe 26 Novemba mwaka kwa lengo la kutathmini hali ya elimu nchini; miaka 50 tangu uhuru wa Tanzania Bara  mwaka 1961.
Hata hivyo pamoja na mafanikio yaliopongezwa na kongamano hilo changamoto mbalimbali  zinazoikabili sekta ya elimu zilibainika, changamoto hizo ni pamoja na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaoshindwa  mitihani, na kuporomoka kwa ubora wa elimu,mfano uwepo wa watoto wanaohitimu darasa la saba bila kujua kusoma na kuandika.
 Aidha,  uhaba mkubwa wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia pamoja na ukosefu wa walimu bora ambao ni muhimu kwa utoaji wa elimu bora bado ni tatizo kubwa.
Changamoto nyingine ni maslahi mabovu ya walimu na watumishi wa ngazi za kawaida mashuleni.
Aliyewahi kuwa Waziri wa Elimu katika serikali ya kwanza, Jackson Makwetta alisema kuporomoka kwa elimu nchini kunatokana na uwepo na viongozi wababaishaji, wasemaji wa maneno mengi bila utekelezaji na kukosa ufuatiliaji.

Kwa upande wake  Dk. Kitila Mkumbo alisema kuwa, kwa sasa taifa lazima liamue kukubaliana na maoni ya wataalamu kuhusu lugha ya kufundishia kama iwe ni Kiswahili, hali aliyosema itawasaidia wanafunzi kuelewa vyema wanachofundishwa darasani,Kama sivyo basi Kiingereza kifundishwe vizuri ili wanafunzi wakielewe na waweze kukitumia ipasavyo.
Kilichosisistizwa na watoa mada na washiriki wa Kongamano hilo ni kuwa, pamoja na kwamba tunastahili kujivunia mafanikio tuliyofikia tangu uhuru lakini ifikie mahala watoto wetu wanapata elimu bora ili waweze kukabiliana na changamoto zinazowazunguka pamoja na jamii zao.
Imefika wakati  badala ya kuendelea kujenga shule mpya, pengine sasa tuangalie zaidi namna ya kuboresha ufundishaji,ufundishwaji pamoja na vitendea kazi kwenye shule zilizopo ili wanafunzi wapate ujuzi wanaohitaji sasa na baadaye katika maisha yao.
Ujuzi au uwezo huo ni pamoja na ule utakaomuwezesha mwanafunzi kujiamini na kujituma, kuweza kutatua matatizo na kukabiliana na changamoto kwa ufanisi na kuchambua na kutathmini taarifa kwa ufasaha na umakini zaidi.
Elimu yetu inapaswa iwape wanafunzi uwezo wa kutumia mitazamo waliyojifunza kwenye eneo moja katika maeneo mengine pamoja na kuwapa  uwezo wa kuelewa na kuwa tayari kuchangia mahitaji ya jamii zao na taifa kwa ujumla.
Dk. Hillary Dachi yeye alizungumzia zaidi kuporomoka kwa hadhi ya ualimu tangu nchi ilipopata uhuru kiasi kwamba sasa hivi walimu wanaishi maisha ya dhiki na wengi hawaipendi kazi hiyo.
Ualimu umepoteza hadhi na heshima yake katika jamii,ni kazi ambayo kwa vijana wengi ni chaguo lao la mwisho,mfano imezoeleka sana nchini kwa mtoto asipo-fanya vizuri (akifeli) akapata madaraja ya chini sana anatafutiwa kozi ya ualimu.
Walio wengi, taaluma ya ualimu ni kama suluhisho la maisha kwamba unapokosa kila kitu, anakuwa huna jinsi ila ni kukimbilia kujifunza ualimu.
Na kwa sababu ukiwa katika ualimu ni rahisi sana kujiendeleza, kwa hiyo walio wengi wanabadilisha taaluma wanaenda katika taaluma nyingine.  
Hali hii inasababisha ugumu wa kupata walimu wa kutosheleza kwa sababu hakuna namna yeyote tunayoifanya kama serikali kuhakikisha kwamba walimu wanaipenda kazi yao, wanaendelea kufundisha na wanapenda kufahamika kama walimu.
Dk. Dachi alitoa angalizo kuwa taifa halitapata walimu wa kutosha ikiwa hakuna juhudi za makusudi za kumfanya mwalimu aliyepo aendelee kufanya kazi yake kwa moyo mmoja na kwa kujituma.
Kukosekana kwa Bodi ya taaluma ya ualimu ambayo ingeweza kusajili walimu na kusimamia maadili na mambo mengine yanayohusiana na taaluma ya ualimu pia imebaki kuwa changamoto kubwa. 
Maoni kama haya ya wadau wa elimu ni vyema yakapewa nafasi stahiki ili kulinusuru sekta hii muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu.
Aidha wenye dhamana ya kusimamia elimu nchini,wadau wa elimu na watanzania kwa ujumla ni sharti tushikamane na kila mmoja kuwajibika katika nafasi yake ili kuinusuru elimu yetu kwa mustakabali wa vizazi vyetu naTaifa kwa ujumla.
0764-784649
zankibindo@gmail.com




0 comments:

 
Top