VIWANJA
SABA VAFUNGIWA KUTUMIWA KATIKA MICHEZO YA LIGI
KUU
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) imefungia
viwanja saba vilivyokuwa vikitumiwa na timu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) hadi vitakapofanyiwa marekebisho ili kukidhi
mahitaji ya mechi za mpira wa miguu.
Uamuzi huo umefikiwa na TPL Board
katika kikao chake cha kwanza kilichofanyika juzi (Novemba 10 mwaka huu) jijini
Dar es Salaam
ambapo pamoja na mambo mengine kilipitia ripoti za mechi za VPL na FDL katika
mzunguko wa kwanza.
Viwanja vilivyofungiwa na marekebisho
yanayotakiwa kufanyika kwanza ili viruhusiwe kutumika tena ni Uwanja wa Kaitaba
mjini Bukoba (majukwaa yake yamechakaa, hivyo kuhatarisha usalama wa
watazamaji), na Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga (vyumba vya wachezaji kubadilishia
nguo (dressing rooms) havina hadhi).
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini
Mbeya (sehemu ya kuchezea- pitch ni mbovu), Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh
Kaluta Amri Abeid jijini Arusha (pitch ni mbovu), Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi
(vyumba vya kubadilishia kutumika kwa ajili ya shule ya awali), Uwanja wa
Majimaji mjini Songea (pitch ni mbovu) na Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro
(pitch ni mbovu).
Klabu ambazo timu zake zinatumia
viwanja hivyo zimeshaarifiwa rasmi juu ya uamuzi huo ambapo ama vinatakiwa
kuwasiliana na wamiliki wa viwanja hivyo ili wafanye marekebisho au kutafuta
viwanja vingine vya kuchezea mechi zao.
Kwa upande wa ripoti za mechi za VPL; Mbeya City
imepigwa faini ya sh. 500,000 na kupewa onyo kali kwa timu yake ya U20 kutocheza
mechi ya utangulizi walipocheza na Yanga. Pia wanatakiwa kulipa gharama za
uharibifu baada ya washabiki wao kuvunja kioo cha basi la Yanga baada ya
gharama hizo kuthibitishwa na Bodi ya Ligi.
Pia
Mbeya City
imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa washabiki wake kushambulia basi la wachezaji
wa Tanzania Prisons baada ya
mechi dhidi yao,
na kulipa gharama za uharibifu baada ya kuthibitisha na Bodi ya Ligi.
Coastal Union imepigwa faini ya sh.
500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake ilipocheza na Azam kwenye Uwanja
wa Mkwakwani ambapo mwamuzi msaidizi Hassan Zani alishambuliwa kwa mawe na
kujeruhiwa mkononi na kichwa, tukio lililosababisha mchezo kusimama kwa dakika
tatu.
Beki wa Coastal Union, Hamad Khamis wa
Coastal Union amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga kichwa kwa makusudi
Kipre Tchetche wa Azam. Kitendo hicho kilisababisha refa amtoe nje kwa kadi
nyekundu, hivyo atakosa mechi tatu zinazofuata za timu yake.
Mchezaji Cosmas Lewis wa Ruvu Shooting
alifanya kitendo cha utovu wa nidhamu kwa kupiga kelele wakati mgeni rasmi
akisalimia timu na kukataa kupeana mkono na kamishna kwenye mechi dhidi ya
Rhino Rangers, hivyo amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000.
Mtunza vifaa (Kit Man) wa JKT Ruvu,
Selemani Oga aliondolewa kwenye benchi la ufundi wakati wa mechi yao dhidi ya Mbeya
City kwa kosa la kutoa lugha chafu kwa
refa, hivyo suala lake
litapelekwa katika Kamati
ya Maadili. Kocha Msaidizi wa Oljoro JKT, Fi
kiri Elias amepigwa faini ya sh. 500,000 na
kufungiwa mechi tatu kwa kumshambulia kwa matusi refa wakati wa mechi yao dhidi ya Ashanti
United. Naye mtunza vifaa wa timu hiyo Elas Justin amepelekwa Kamati ya Maadili
kwa kumshambulia refa kwa matusi ya nguoni.
Simba wamepigwa faini ya sh. 500,000
kutokana na vurugu za washabiki wake wakati wa mechi dhidi ya Kagera
Sugar.
Katika FDL, mchezaji Ally Mtoni wa
Villa Squad amepigwa faini y ash. 200,000 na kufungiwa mechi tano. Kosa lake ni
kujisaidia haja ndogo golini wakti wa mechi dhidi ya Ndanda FC iliyochezwa
mjini Mtwara.
Kamishna Paul Opiyo wa mechi ya FDL
kati ya Villa Squad na Transit Camp kwa kutokuwa makini. Katika ripoti yake
ameeleza kuwa Transit Camp ilichelewa kufika uwanjani, lakini hakusema
ilichelewa kwa muda gani.
Kocha wa Polisi Dar
es Salaam, Ngelo Nyanjabha na Meneja wa timu hiyo Mrimi Masi
wamepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi tatu kila mmoja kwa kuongoza
kundi la washabiki kumvamia refa wa mechi yao
dhidi ya Villa Squad iliyochezwa Dar es Salaam.
Pia Bodi ya Ligi imeagiza Polisi
waandikiwe barua ya onyo kwa vile wakati waamuzi wanapigwa walikuwepo lakini
hawakutoa msaada kwa wakati.
Kocha wa Friends Rangers, Kheri Mzozo
amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi sita kwa kosa la kumtukana refa
na kutishia kuhamamisha washabiki waingie uwanjani kufanya fujo kwenye mechi
dhidi ya Villa Squad.
Naye Kocha msaidizi wa timu ya Transit
Camp, Haji Amiri amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi sita kwa
kutoa lugha ya matusi kwa mwamuzi wa akida wakati wa mechi dhidi ya Friends
Rangers.
Adhabu zote zimetolewa kwa mujibu wa kanuni. Pia Bodi ya Ligi imeahirisha kufanya uamuzi wa mechi kati ya Stand United na Kanembwa JKT iliyochezwa Uwanja wa Kambarage ili kukusanya taarifa zaidi. Mechi hiyo haikumalizika. Bodi ya Ligi itakutana tena Jumapili (Novemba 17 mwaka huu).
0 comments:
Post a Comment