RAIS
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amemtambulisha
winga wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, Emmanuel Amunike kuwa kocha
mpya wa timu ya taifa, Taifa Stars.
Karia amemtambulisha Amunike mwenye umri wa miaka 47 katika mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika hoteli ya New Africa mjini Dar es Salaam jioni hii baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili.
Amunike
aliyeng’ara na Super Eagles katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994
nchini Marekani akicheza wingi ya kushoto, mtihani wake wa kwanza
utakuwa ni mchezo dhidi ya Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala,
kabla ya kuwafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za
mzunguko wa kwanza kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Taifa
Stars inakuwa timu ya kwanza ya taifa ya wakubwa Amunike kufundisha,
baada ya awali kuwa kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya
kwao, Nigeria kuanzia mwaka 2014 hadi 2017.
Zaidi ya hapo, Amunike mwenye umri wa miaka 47 amefundisha klabu za Al Hazm ya Saudi Arabia, kama Kocha Msaidizi mwaka 2008 kabla ya kuhamia Julius Berger hadi mwaka 2011 alipojiunga na Ocean Boys, zote za Nigeria.
Alipoachana
na U-17 ya Nigeria akaenda kufundisha Al Khartoum SC ya Sudan kuanzia
mwaka 2017 hadi 2018 na sasa anakuja kuujaribu ‘mfupa’ uliowashinda
wengi, Taifa Stars.
Kisoka,
Amunike aliibukia klabu ya Concord mwaka 1990 kabla ya kwenda kuchezea
Julius Berger 1991, zote za kwao, Nigeria baadaye Zamalek ya Misiri
mwaka 1991 hadi 1994 ndipo akahamia Ulaya.
Alianza
na klabu ya Sporting CP ya Ureno kuanzia 1994 hadi 1996 kabla ya
kuhamia Barcelona ambako alicheza hadi mwaka 2000 alipohamia Albacete
zote za Hispania na mwaka 2003 alijiunga na Busan I’Cons ya Korea Kusini
alikocheza hadi 2004 akahamia Al-Wehdat ya Jordan kumalizia soka yake.
TAFADHARI TOA MAONI YAKO HAPA
0 comments:
Post a Comment