Tumepokea kwa matumaini mema
mikakati mbalimbali iliyotangazwa na Rais John Pombe Magufuli (JPM) ya
kuimarisha mapato ya Serikali kwa kukusanya kodi zaidi na kupunguza matumizi ya
fedha ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku safari za nje ya nchi
Hii inatokana na ukweli kwamba
serikali yoyote duniani inahitaji fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo;
kugharimia huduma za afya, elimu, ujenzi wa miundombinu ya usafiri, viwanda na
maeneo ya uzalishaji.
Hivyo ili kuhakikisha hayo
yanafanyika kama ilivyoelezwa katika Ilani ya Uchaguzi, JPM aliweka wazi
mikakati hiyo alipokutana na makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, Gavana wa
Benki Kuu (BoT), Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuwasisitizia
mkazo mkubwa ni kuongeza mapato.
Baadhi ya mikakati hiyo ni TRA
kuongeza makusanyo ya kodi, kuwabana wafanyabiashara wakubwa na kuacha kutoa
ovyo misamaha ya kodi ili kila mfanyabiashara aweze kulipa kodi kulingana na
aina na ukubwa wa biashara yake. Lengo la mkakati huu ni kuondokana na
utaratibu uliozoelekea wa kuwabana zaidi wafanyabiashara wadogo na wa kati,
ilhali wakubwa wakikwepa kwa mbinu mbalimbali zikiwamo za kupewa misamaha.
Mikakati mingine iliyotajwa wakati
wa kikao hicho ni kupiga marufuku safari za nje ya nchi kwa watendaji wengi na
kwamba shughuli ambazo wangepaswa kwenda kuzifanya, kuanzia sasa zitahitaji
kibali cha JPM au zitafanywa na mabalozi wa Tanzania walioko katika nchi
husika.
0 comments:
Post a Comment