TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inatarajia kutumia mfumo mpya wa kielektroniki katika kujumlisha matokeo ya kura kwa lengo la kuondoa makosa mbalimbali ya kibinadamu, yanayoweza kutokea kwa bahati mbaya wakati wa kujumlisha matokeo hayo katika uchaguzi mkuu.
Mfumo huo mpya wa Menejimenti ya Matokeo (RMS), unatumia mashine za kisasa zenye uwezo wa kuchapisha na kunukushi karatasi za kupigia kura zaidi ya 60 kwa dakika moja.
Mkurugenzi wa NEC, Kailima Kombwey alisema jana kwamba Oktoba 11, mwaka huu, waliwaalika wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kutoka vyama vyote vya siasa na mfumo huo ukapitishwa.
Akiwasilisha mada ya maandalizi ya uchaguzi, Kombwey alitaja makosa yanayoweza kutokea katika kujumlisha kura ni pamoja na matokeo ya kituo kimoja, kujumlishwa zaidi ya mara mbili, kukosea uandikaji wa namba na usahihi wa ujumlishaji.
“Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 mfumo huu ulisanifiwa upya na kutumika, hata hivyo kasoro chache zilioneshwa. Kwa uchaguzi wa mwaka huu, tume imeboresha mfumo huu na kuondoa upungufu katika maeneo yote yaliyokuwa na changamoto mwaka 2010,” alisisitiza Kombwey.
Alisema pamoja na mfumo huo, pia tume hiyo imeandaa mfumo mbadala, alioutaja kuwa ni Spreadsheet Excel RMS, ambao utatumika iwapo kutakuwa na changamoto katika kutumia mfumo uliondaliwa.
Aidha alisema tume hiyo inafanya maandalizi ya kutumia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa ajili ya kutuma matokeo yote, badala ya kutumia mtandao wa simu za mkononi. “Katika uchaguzi wa mwaka 2010, utumaji wa matokeo ulikuwa na changamoto nyingi. Kati ya majimbo 239 ni majimbo 150 tu yaliweza kutuma matokeo kwa mfumo uliokuwa umeandaliwa, ambao ni kupitia mtandao wa simu za mikononi, matokeo yaliyobaki yalitumwa kwa nukushi ,” alifafanua.
Alisema kitendo cha kutumia mkongo huo wa taifa, kitasaidia upatikanaji wa matokeo mapema kama inavyokusudiwa, ingawa pia njia mbadala ya kutuma matokeo kwa nukushi imeandaliwa na halmashauri zote zimepatiwa vifaa, vitakavyowezesha utumaji wa matokeo kwa haraka kufanyika.
Aidha, tume imekubaliana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuhusu kutumia Mkongo wa Mawasiliano wa Tamisemi, kusaidia utumaji wa taarifa za matokeo kutoka katika halmashauri hadi NEC. Kuhusu elimu, Kombwey alisema jumla ya asasi za kiraia 451 ziliomba kutoa elimu ya mpiga kura.
Kati ya hizo ni asasi 447 zilikidhi vigezo na hivyo kupewa kibali cha kutoa elimu hiyo. Alisema asasi hizo zimesaini Maadili ya Utoaji wa elimu ya Mpiga kura na kukubali kutumia mwongozo wa Elimu ya Mpiga kura.
0 comments:
Post a Comment