MAJAMBAZI 10 wanaounda mtandao hatari wa uhalifu nchini, wametiwa mbaroni wakati wa msako mkali uliofanikisha pia kukamatwa kwa silaha mbalimbali.
 
Silaha hizo ni bunduki tisa zikiwemo SMG tatu, bastola mbili, short gun nne na risasi 15 zilikamatwa.


Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliyasema hayo ofisini kwake kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Kova aliyataja majina ya wahalifu hao kuwa ni, Maulid Mbwate (23), Foibe Vicent (30), Vincent Kadogoo (30), Said Mlisi (29) na Hemed Zaga wote wakazi wa Dar es Salaam.
Wengine ni Mohamed Said (31), Lucy Mwafongo (41), Rajab Ramadhan (22), Deus Chilala (30) na Marietha Mussa (18), pia wa Dar es Salaam.  
 
Alisema kutokana na matukio kadhaa ya kihalifu likiwemo la wizi kwenye benki ya Stanbic tawi la Kariakoo Sokoni, polisi imejizatiti kuendelea na operesheni kabambe bila kulala.
 
Kova alisema mpaka sasa hakuna aliyekamatwa kuhusika na uhalifu huo uliotokea juzi mchana, na kwamba wanaendelea kuwasaka majambazi wote watano waliohusika.
 
Akielezea tukio hilo alisema, kutokana na upelelezi wao majambazi hao hawakuweza kuiba fedha za benki kutokana na mfumo mzuri wa usalama ulioko kwenye benki hiyo, hivyo waliiba fedha za wateja waliokuwa wakisubiri huduma ya kuweka fedha.  

"Benki ile ina 'system' nzuri ya usalama vikiwemo ving'ora na milango inayotumia kadi kwa hiyo hawakuweza kuingia ndani kunakohifadhiwa pesa. Baada ya kushindwa kufanya hivyo, watumishi wa benki wakaminya ving'ora ndipo wakakimbia na fedha za wateja," alisema Kova.

Aidha Kamanda Kova alisema kiasi cha fedha zilizoibwa kwenye wizi huo wa benki ya Stanbic hakijafahamika mpaka upelelezi utakapokamilika.
Pia alisema kutokana na tukio hilo benki zote zinatakiwa kuiga mfano huo kwa kufunga mifumo mizuri ya usalama ikiwa ni pamoja na kamera, mashine za kutambua chuma ambayo hutambua silaha kama visu na bunduki mara mtu anapoingia nazo ndani ya benki husika.
Kwa kuongezea Kova alisema jeshi la polisi linaruhusu benki yoyote kuingia mkataba nao ili badala ya kulindwa na kampuni za ulinzi, ziweze kulindwa na jeshi hilo ambapo ulinzi huwa thabiti na matukio ya kihalifu kama hayo huwa hayatokei mara kwa mara.
 
Kuhusu sikukuu ya Idd el Fitr, Kamishna Kova alisema vikosi vyote vya Jeshi la polisi vimejipanga kuweka ulinzi kila eneo la mkoa wa Dar es Salaam kwa kuweka vituo vya polisi vya muda sehemu ambayo havipo.
 
Aidha aliwataka wananchi wawe makini na matumizi ya barabara kwa kuzingatia sheria na kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa haraka kuhusiana na shaka yoyote wanayoweza kumtilia mtu au kitu kilichopo kwenye maeneo yao.

0 comments:

 
Top