Tanzania imesema
hataitajitoa katika Jumuiya ya Afrika kama wengi walivyodhani na badala yake
imedhamiria kuhakikisha Jumuiya hiyo inadumu na kustawi daima.
Akilihutubia bunge la Tanzania, mjini
Dodoma, Rais Jakaya Kikwete amesema kwamba
Tanzania haina mpango wala fikra za kujitoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
kwa kuwa ni nchi inayoamini katika umoja na maendeleo na imekuwa ikitumia
gharama kubwa kuhakikisha jumuiya hiyo inaimarika.
"Tanzania ni mwanachama mvumilivu,
mtiifu na mwaminifu na tunatimiza wajibu wetu kwa jumuiya na kuhusika
kikamilifu katika ujenzi wake." amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete ametumia muda mrefu katika
hotuba hiyo kuchambua masuala mbalimbali ya msingi ya uhai wa jumuiya hiyo huku
akisema ameshangazwa na nchi za Kenya, Uganda na Rwanda kuzitenga Tanzania na
Burundi.
Amesema kuna masuala ambayo hayazifungi
nchi wanachama katika mkataba wa umoja wao, hivyo kuwa na uhuru wa ushirikiano
na nchi ndani ya jumuiya na hata nje.
"Naomba kwanza niweke wazi jambo moja,
kwamba nchi mbili wanachama au zaidi hazikatazwi kuwa na makubaliano ya
ushirikiano katika kufanya mambo mbalimbali. Hata sisi Tanzania tunao
ushirikiano wa namna hiyo na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Lakini, nchi wanachama zinatakiwa kufanya hivyo kwa yale mambo
ambayo hayako kwenye shughuli za Jumuiya kwa maana kwamba hayamo katika Mkataba
au Itifaki au hakuna uamuzi wa msingi uliofanywa na vikao au taasisi za Jumuiya
kuyashughulikia. Pia, tunaweza kufanya hivyo kwa mambo ambayo yalishaamuliwa na
Jumuiya yatekelezwe na ruhusa imetolewa kwa nchi yo yote iliyokuwa tayari
kutekeleza ama peke yake au kwa kushirikiana na nchi nyingine".
Aidha Rais Kikwete amesema huenda mambo
yanayoitenga Tanzania na nchi nyingine tatu za jumuiya ya Afrika Mashariki, ni
msimamo wake kuhusu kuharakisha shirikisho, masuala ya ardhi, ajira, na
uhamiaji.
Hata hivyo Rais Kikwete amesema Tanzania
haina mpango wa kujitoa kwa kuwa inaamini na ina uhakika kuwa haijafanya jambo
lolote baya dhidi ya jumuiya au nchi mwanachama yeyote wa jumuiya hiyo.
0 comments:
Post a Comment