Utawala wa Rais John Magufuli umebainisha mambo 10 yaliyofanyika katika kipindi cha miaka miwili tangu ulipoingia madarakani.

Rais Magufuli aliapishwa kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano Novemba 5,2015 akichukua nafasi iliyoachwa na Rais Jakaya Kikwete aliyehudumu kwa miaka 10 kuanzia 2005-2015.

Akitoa tathimini ya utawala huo leo Jumapili Novemba 5,2017 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi amesema ndani ya miaka miwili mengi yamefanyika ambayo ameyagawa katika maeneo 10.

Mosi, Dk Abbasi amesema uwajibikaji wa watumishi wa umma na wananchi kwa jumla umekuwa mkubwa kwa kuwa kumekuwepo na ari ya kufanya kazi.

Pili, amesema ni msukumo ambao Serikali imeweka katika ukusanyaji wa kodi na kinachopatikana kinatumika ipasavyo.

"Zaidi ya Sh236 bilioni ziliokolewa kutoka kwa walipa kodi zilizokuwa zinawalipa watumishi hewa, tumeondoa watumishi wenye vyeti feki. Zaidi ya Sh142 bilioni nazo zimeokolewa kutoka kwa watumishi walioghushi vyeti na zote zimeelekezwa kutatua kero za wananchi," amesema Dk Abbasi.

Tatu, amesema vita ya ufisadi imekuwa kubwa na imesaidia kuleta mageuzi na fedha ambazo zimekuwa zikiokolewa kutokana na vita hiyo zinaelekezwa kwa wananchi kupitia miradi ya maendeleo.

"Kuna Mahakama ya mafisadi imeanzishwa, kesi zake zinaanzia ngazi ya chini na mpaka sasa kuna kesi tatu, mbili ziko Dar es Salaam na moja iko Mtwara na zingine 107 ziko ngazi za chini zinashughulikiwa," amesema.

Nne, amesema, "Serikali inavyopigania rasilimali za Taifa. Vita katika eneo la madini tumefanya kupitia upya mikataba na kubwa tumejitambua kama Taifa na sasa wawekezaji wanajua Tanzania ukienda lazima uheshimu sheria."

Tano, Dk Abbasi amesema uamuzi mgumu lakini makini uliofanywa na Serikali ingawa wapo waliopinga na kueleza haiwezekani, lakini imewezekana.

"Watumishi kutokwenda nje ya nchi, kati ya mwaka 2014/15, Sh216 bilioni zilitumika lakini kwa miaka miwili hii ni Sh25 bilioni pekee ndizo zimetumika. Mimi nimesafiri mara mbili tu," amesema akizungumzia moja ya uamuzi huo.

Amezungumzia azma ya Serikali kuhamia Dodoma akisema imefanikiwa kwa sehemu kubwa na tayari Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yupo Dodoma. Amesema mwaka huu Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan atahamia na mwakani atakuwa ni Rais Magufuli.

Sita, ametaja ni azma ya nchi kujitegemea akisema wananchi wanafanya kazi ili kutekeleza hilo. Amesema ukusanyaji mapato umeongezeka kutoka Sh9.9 trilioni hadi Sh14 kwa mwaka.

Saba, amesema miradi mikubwa inatekelezwa kama vile ujenzi wa reli ya kisasa na uboreshaji wa shirika la ndege, akisema ununuzi wa ndege umefanyika na  hadi Julai,2018 zitakuwa zimewasili nchini.

Nane, amesema Serikali imeongeza bajeti katika maeneo muhimu ya sekta za afya, elimu bure na miundombinu ya barabara.

"Kumekuwepo na upatikanaji wa dawa katika hospitali zetu ukilinganisha na awali, hii inasaidiwa na mkakati wa Serikali wa kununua dawa moja kwa moja kwa wazalishaji na bajeti ya Wizara ya Afya imeongezeka kutoka Sh30 bilioni hadi Sh261 bilioni, yote haya ni mafanikio ya miaka miwili," amesema.

Tisa, Dk Abbasi amesema Rais Magufuli amekuwa akiahidi na kutekeleza.

Kumi, amesema suala la Tanzania ya viwanda licha ya kueleza ni gumu lakini ni lazima nchi ielekee huko.

TAFADHARI TOA MAONI YAKO HAPA

0 comments:

 
Top