Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amelaani kitendo cha watu wanaosadikiwa kuwa ni majangili kumuua kwa kumpiga risasi Rubani wa helkopta Kepteni Roger Gower, raia wa Uingereza na kisha kuidondosha helkopta aliyokuwa akiiendesha wakati alipoungana na Askari wa wanyamapori waliokuwa wakikabiliana na majangili katika pori la akiba lililopo katika wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu.

Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa sana na tukio hilo na ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha waliomuua Kepteni Gower na kuidondosha helkopta aliyokuwa akiiendesha wanakamatwa na wanafikishwa mikononi mwa vyombo vya sheria.

Amemtumia salamu za pole, Balozi wa Uingereza hapa nchini kwa kumpoteza raia wake ambaye alikuwa akitoa mchango mkubwa katika kuhifadhi wanyamapori wa hapa nchini Tanzania.

Aidha, Rais Magufuli amesema serikali yake itahakikisha inaendeleza mapambano dhidi ya ujangili kwa nguvu zake zote na kuwataka wananchi na wadau mbalimbali wa hifadhi ya wanyamapori, kutokatishwa tamaa na tukio hili na watoe ushirikiano wa kutosha kuwafichua watu wote wanaojihusisha na ujangili ama biashara ya bidhaa zitokanazo na ujangili.

Katika tukio hilo, pamoja na kumuua Kepteni Roger Gower watu hao wanaosadikiwa kuwa majangili wamemjeruhi Askari wanyama pori mmoja na wamewaua tembo watatu.

Gerson Msigwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
Dar es salaam
31 Januari, 2016
















AHSANTE KWA KUTEMBELEA BLOGU HII,UNAWEZA KUTOA MAONI YAKO PIA

0 comments:

 
Top