Namshukuru Mwenyezi Mungu aliyeiwezesha nchi yetu kutimiza miaka 54 ya uhuru kwa salama na amani. 
 
Namshukuru Mungu pia kwa kuniwezesha kuiona siku hii nikiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
 
Napenda kuchukua fursa hii, kuwapongeza Watanzania wenzangu kwa Taifa letu kutimiza 54 ya Uhuru tarehe 09 Desemba, 2015.
 
Napenda kuwahakikishia kwamba, kama ilivyokuwa kwa Serikali za awamu zilizopita, Serikali ya Awamu ya Tano itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuhakikisha kwamba Uhuru, Amani na Umoja na wa Taifa letu hauchezewi na mtu, kikundi au Taifa lolote.
 
Tutaendelea kudumisha Uhuru wetu na Mapinduzi ya Zanzibar, tunu ambazo ni msingi wa Muungano wetu na Utanzania wetu.

Tofauti na ilivyozoeleka tumeamua mwaka huu kusherekea kumbukumbu hizi kwa kufanya kazi,. Wakati tunapata Uhuru Taifa letu lilikuwa likiongozwa na kauli mbiu ya UHURU NA KAZI. 
 
Kauli hii ilikuwa na lengo la kuamusha moyo na uzalendo wa kufanya kazi miongoni mwa Watanzania kwa kutambua kuwa uhuru wetu hautakuwa na maana kama hatutafanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kujenga Taifa linalojitegemea.
 
 Watanzania katika miaka ile waliitikia wito huo kwa kufanya kazi za kuwaongezea kipato na za kujitolea katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwaletea maendeleo.
 
 Katika miaka ya hivi karibuni moyo na uzalendo wa kufanya kazi miongoni mwetu umepungua sana. Kwa sababu hiyo, niliamua kutumia siku ya kumbukumbu za uhuru wetu mwaka huu kukumbushana na kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya UHURU NA KAZI kwa kufanya kazi hususan ya usafi wa mazingira. Madhimisho ya Uhuru mwakani yatasherehekewa kama kawaida.

Nawapongeza viongozi wa Mikoa na Wilaya na wa Taasisi za umma na binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyojitokeza katika kuhakikisha kuwa zoezi la usafi wa mazingira linafanikiwa.

Napenda kutoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaweka mifumo na taratibu thabiti zitakazowezesha usafi wa miji yetu kuwa endelevu. 
 
Viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri waache visingizio, uwezo na mamlaka ya kuhakikisha kwamba usafi katika miji yao unadumishwa wanao. Uwezo wa utendaji wao utapimwa pia kutokana na hali ya usafi wa miji yao.

Naomba wananchi tushirikiane katika kuhakikisha kuwa nyumba na mazingira ya nyumba zetu yanakuwa safi na maji ya kunywa katika maeneo ambayo hayawekwi dawa yanachemshwa.
 
 Aidha, wananchi wajizuie kutupa taka ovyo na viongozi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wahakikishe kwamba kila nyumba inakuwa na choo.
 
 Tutashinda vita dhidi ya maradhi kama kipindupindu ikiwa sote tutazingatia kanuni za afya. Kila mtu atimize wajibu wake.

Mwalimu alisema Uhuru na Kazi na mimi nasema Hapa Kazi Tu.

0 comments:

 
Top