Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, amewasimamisha kazi watumshi watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, kutokana na kuruhusu ujenzi wa nyumba juu la bomba la mradi wa maji na kuamuru ivunjwe mara moja.

Mulongo alitoa maagizo hayo jana baada ya kuitisha kikao cha dharura cha wakuu wa idara ya halmashauri hiyo kutaka kufahamu chanzo cha ujenzi wa nyumba hiyo baada ya kupata taarifa ya mradi wa maji ulioanza mwaka 2005 na kugharimu Sh. bilioni 20.

“Kuanzia sasa natoa agizo la kuwasimamisha kazi watendaji watatu wa halmashauri ambao ni Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira, Nestory Kabete, Kaimu Afisa Ardhi, Richard Pungu, pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Mipango Miji, Wilson James, baada ya kushindwa kutekeleza kazi walizopewa na serikali,” alisema Mulongo.

Alisema watumishi hao kwa pamoja walipuuzia na kukaidi amri ya serikali waliyoitoa ya siku 21 ya kubomoa nyumba iliyojengwa juu ya mradi wa maji inayomilikiwa na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Pamphil Masashua, tangu Juni mwaka huu, hali iliyosababisha mradi huo wa maji kusuasua.

Alisema wataalam wa maji na ardhi wanatakiwa kwenda ofisi za mkoa huo kuanzia jana ili wafanyie uchunguzi wa kina na iwapo watabaini nyumba hiyo ni mali ya Masashua na imejengwa juu ya miundombinu ya maji lazima ibomolewe haraka.

“Na yeyote aliyeshiriki katika kutoa kibali cha ujenzi na ramani ambavyo havikuwa sahihi, lazima watafikishwa mbele ya mahakama,” alisema. 

Aidha, Mulongo alimtaka katibu tawala wa mkoa huo, kuwahamisha watumishi wa idara ya ardhi pamoja na wanasheria wa halmashauri hiyo kwa kufanya kazi kwa mazoea na kusababisha wananchi kubuni mbinu mbadala za kuhujumu serikali.

Katika hatua nyingine, Mulongo alimuagiza Mkurugenzi wa Wilaya ya Sengerema, Julius Chaliya, na Katibu Tawala, Ndaro Kulijila, kuhakikisha wanawalipa walimu 234 pesa zao za mishahara ikiwa ni pamoja na barua za kuwaidhinisha kupanda vyeo kuanzia 2014/15 haraka.

0 comments:

 
Top