WAFUGAJI waliovamia maeneo ya wakulima katika kijiji cha Dihinda wilayani Mvomero mkoani Mogorogo na kusababisha mapigano yaliyoua mkulima na ng’ombe 71, wamekimbia kijijini hapo na kutokomea kusikojulikana.

Akizungumzia hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Wilaya ya Mvomero, Mkuu wa Wilaya hiyo, Betty Mkwasa alisema ulinzi bado umeimarishwa eneo hilo, na kwamba wafugaji waliovamia wamekimbia.

“Wafugaji wamekimbia na sisi tutateketeza maboma yao, kwa sababu walivamia eneo hili la wakulima na ng’ombe walioachwa wamepigwa mnada na fedha imeingizwa kwenye mfuko wa serikali ya kijiji hicho,”alisema Mkwasa.

Aidha, katika msako uliofanywa kwa ushirikiano wa Serikali ya Wilaya na Polisi silaha moja ya askari iliyochukuliwa ilipatikana na kwamba wakulima wametolewa hofu na kusisitizwa kuendelea na kazi zao kama kawaida.

Alifafanua kwamba hali kwa sasa kijijini hapo ni shwari na kwamba mifugo iliyouawa kwa kukatwakatwa mapanga yote imeshafukiwa na uongozi wa serikali ya wilaya umepanga kuingia mkataba na viongozi wa vijiji na kata ili kudhibiti, migororo baina ya makundi hayo.

Alisema katika kudhibiti matukio ya mapigano au uvunjifu wa sheria na mpango wa matumizi bora ya ardhi, Mvomero itaanza kuingia mkataba na watendaji wa vijiji na kata na iwapo migogoro itatokea, wao ndio watawajibishwa.

Awali Desemba 12, mwaka huu, kundi la wafugaji wa jamii ya Kibarbaig waliwavamia wakulima na kuanza kuwashambulia kutokana na mmoja wa wafugaji ambaye mifugo yake iliharibu mazao ya mkulima kutakiwa kulipa fidia ya Sh 200,000.

0 comments:

 
Top