Kufuatia maagizo ya Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa hivi karibuni ya kusitisha safari za nje kwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imeanza kutekeleza maagizo hayo kwa kutoa maelekezo mahsusi kwa Balozi zake nje.

Wizara imezielekeza Balozi zote zilizopo maeneo mbalimbali duniani kujipanga ili kushiriki kikamilifu katika kuiwakilisha Serikali kwenye mikutano yote ya kimataifa na kikanda inayofanyika katika maeneo yao ya uwakilishi. Tanzania inazo Balozi 35; Balozi Ndogo tatu; Vituo viwili vya Biashara; na Konseli za Heshima 17 katika nchi mbalimbali. Hizi zote zitahusika katika kuendeleza utekelezaji wa Diplomasia yetu ya Uchumi na uwakilishi wa maslahi ya nchi yetu.

Aidha, hadi sasa Mikutano ambayo tayari imefanyika na Balozi zetu kuwakilisha ni pamoja na Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) unaoendelea nchini Malta na Mkutano wa Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Habari wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika nchini Lesotho.

Aidha, Wizara inatoa wito kwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali kuwasilisha mapema taarifa za mikutano inayohusu sekta zao ili kutoa fursa kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuzifanyia kazi kwa wakati ili kuhakikisha ushiriki wa Tanzania unakuwa wenye tija kwa taifa.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inaungana na wadau wengine kumpongeza Mhe. Rais Magufuli kwa hatua anazozichukua za kuleta ufanisi mkubwa wa kazi na kubana matumizi ili kuiwezesha Serikali kuwahudumia wananchi kikamilifu.

Imetolewa na:
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
27 Novemba, 2015

0 comments:

 
Top