Baada ya kufafanua maeneo haya manne ya msingi kuhusu mabadiliko nitakayo yaleta na kuyasimamia, sasa naomba niingie kwa undani kuhusu mambo ambayo Serikali nitakayounda itatekeleza ni mambo 16.
Kwanza, Serikali nitakayoongoza itapambana na umaskini, ujinga na maradhi kikamilifu.
Itaboresha elimu kama hatua ya kwanza ya kuwapa Watanzania uwezo wa kujikomboa. Kila Mtanzania atapata elimu bora itakayogharimiwa na serikali kutoka ngazi ya elimu ya awali hadi Chuo Kikuu.
Tutapiga marufuku michango kama vile ya kujenga maabara na tutaboresha maslahi na vitendea kazi kwa waalimu na kurudisha posho ya kufundishia.
Tutapanua wigo wa mafunzo ya kijeshi na kujitegemea yanayotolewa katika Jeshi la Kujenga Taifa kwa kuongeza idadi ya wanaojiunga mara tano zaidi kuliko ilivyo sasa ili kuboresha mafunzo ya stadi za maisha, ufundi na ujasiriamali.
Pili, tutaondoa kodi zote za kero kwa wafanya biashara hususani wafanya biashara wadogo wadogo, mama lishe, boda boda, na machinga.
Aidha, tutaondoa kodi zote za mazao kwa wakulima, wafugaji, na wavuvi wadogo wadogo ili tuongeze kipato na uwezo wao wa kuwekeza na kuliwezesha Taifa kujitosheleza kwa chakula na lishe bora.
Tutahakikisha kuwa elimu inatolewa kwa makundi haya ili kuinua kiwango cha uzalishaji kwa kusimamia shughuli zao kitaalam kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Vile vile, tutayawezesha makundi haya kwa mikopo ya riba nafuu kutokana na benki mahsusi itakayoanzishwa kusimamia sekta ya ufugaji na uvuvi.
Tatu, tutakuza na kulinda sekta binafsi na bidhaa za ndani kwa kuwapa Watanzania upendeleo wa maksudi ili waimarike na waweze kuhimili ushindani.
Tutawapa upendeleo katika zabuni na manunuzi ya serikali na kuwajengea mazingira mazuri zaidi ya biashara.
Serikali nitakayoongoza itajenga uhusiano wa karibu na wawekezaji katika biashara na viwanda katika kuhakikisha sera na mikakati ya Serikali haipingani na mazingira ya uzalishaji na mienendo ya biashara.
Tanzania ina kodi nyingi kuliko nchi zote Afrika ya Mashariki na zile za SADC. Tutaweka mfumo wa kodi utakaotuwezesha kushindana kimataifa.
Kazi hii ni nzito kwa sababu Serikali ya CCM imeacha dosari kubwa katika mazingira yanayovutia uwekezaji.
Ukweli ni kwamba Tanzania imepoteza uwezo wa ushindani katika soko la ndani na la nje kutokana na ubovu wa miundombinu pamoja na urasimu hali ambayo imesababisha gharama za usafiri na usafirishaji kuwa kubwa kupita kiasi.
Taarifa ya Benki ya Dunia ya mwaka 2015 ambayo hupima ubora wa miundombinu ya usafiri kwa madhumuni ya biashara inaonyesha kwamba kati ya nchi 160 zilizofanyiwa utafiti, Tanzania imeshika nafasi ya chini ya 138.
Hata nchi zinazopitisha bidhaa zao Tanzania (landlocked) kama vile Malawi, Rwanda na Burundi zimeshika nafasi za 73, 80 na 107. Kenya inashika nafasi ya 74.
Nne, tutakuza viwanda vidogo vidogo ili viwe mhimili wa uchumi wa nchi. Lazima tuimarishe uzalishaji na kusindika mazao yetu ili kuongezea thamani na kutengeneza vyanzo vya ajira.
Tano, tutaimarisha mfumo wa afya ya msingi na kuboresha huduma za kinga ili kuepukana na gharama kubwa za tiba.
Serikali nitakayoongoza itaandaa taratibu na mifumo ya kuwapatia wananchi wote huduma za afya na matibabu kupitia bima za gharama nafuu na mifuko ya hifadhi ya jamii.
Tutaimarisha miundombinu ya afya pamoja na kujenga hospitali za kisasa ili kusogeza huduma za afya karibu na jamii na kuepukana na gharama kubwa za tiba za nje ya nchi.
Wazee na wananchi wasiojiweza watapewa posho ya kujikimu inayokidhi mahitaji ya msingi ili waishi kwa heshima ndani ya familia na jamii zao.
Sita, tutadhibiti matumizi serikalini na katika mashirika ya umma kama vile kupiga marufuku matumizi ya magari ya anasa, kupunguza safari za ndani na nje,
usafiri wa anga wa daraja la kwanza na semina na makongamano yasiyo ya lazima.
Watanzania watapewa fursa maalum ya kushiriki katika uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi. Sambamba nahili, Serikali yangu itaanzisha Wizara maalum itakayosimamia nishati ya gesi na mafuta.
Nane tutaimarisha ofisi ya Msajili wa Hazina ili kusimamia vema uwekezaji wa Serikali katika mashirika au makampuni yote ambamo serikali ina hisa na kuipa ofisi hiyo mamalaka kamili.
Tutahakikisha kuwa mashirika ya umma yanaendeshwa kwa misingi ya faida na uadilifu.
Tisa, tutadhibiti vitendo vya rushwa iliyo kithiri katika bandari zetu, ukwepaji kodi za ushuru wa forodha na kupiga marufuku misamaha ya kodi holela ili kuokoa mabilioni ya fedha yanayopotea kila wiki.
Sambamba na hayo, tutarahisisha utaratibu wa kulipa kodi ili kuondoa kero na mazingira ya rushwa. Kwa kudhibiti makusanyo ya kodi tutaweza kupata fedha zaidi za kugharimia huduma za msingi kikamilifu.
Kumi, tutaimarisha utendaji na uwajibikaji katika sekta ya umma na kuhakikisha kuwa rushwa, urasimu na kero zinazodumaza maendeleo ya wananchi zinakomeshwa.
Sambamba na hayo, tutaboresha maslahi na vitendea kazi kwa wafanyakazi wa Serikali na sekta ya umma.
Kumi na moja, tutahakikisha tunatengeneza vyanzo vipya vya ajira kwa kukuza sekta za kilimo, viwanda na utalii.
Kumi na mbili, tutaimarisha miundombinu na kujenga mtandao wa reli tukianza kwa kujenga upya na kwa viwango vya kisasa Reli ya Kati na Reli ya Tanga-Arusha-Musoma.
Pia tutajenga barabara za viwango vya juu kuliko sasa zikiwemo za vijijini ili kuchochea biashara na maendeleo.
Tutaboresha bandari za baharini na maziwani na kujenga zingine mpya kama vitega uchumi vya Taifa ili kurejesha biashara tulizopoteza kwa bandari za nchi jirani. Tutanunua meli mpya za usafiri wa watu na mizigo kwa ajili ya usafiri katika ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Tutajenga upya Shirika la Ndege la Taifa linalojiendesha kwa misingi ya faida.
Tutajenga miundombinu ya kisasa na kuondosha misongamano ya magari hasa katika majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha
Tutasimamia uzalishaji na usambazaji wa umeme mijini, vijijini ili kufikia zaidi ya asilimia sabini na tano ya Watanzania ifikapo mwaka 2020.
Tutasimamia upanuzi na usambazaji wa umeme wa uhakika na kufanya mgao wa umeme kuwa historia hapa nchini.
Kumi na tatu, tutahakikisha Katiba ya wananchi inakuwepo ili kujenga misingi ya demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari na kuwapa nafasi asasi za kiraia, vyombo vya dola, Bunge na wananchi kusimamia uwajibikaji nchini.
Tutasimamia utawala bora kwa kuamini kuwa kama nchi itaendeshwa kwa misingi ya sheria na utawala bora, haki itatendeka, rushwa itadhibitiwa, barabara bora zitajengwa kwa viwango, shule na hospitali bora zitajengwa na kupewa vifaa na kwamba mashirika yetu yataendeshwa kwa tija.
Kumi na nne, tutaimarisha mchango wa wataalam wetu, wanawake na vijana, katika kuandaa sera na kusimamia uchumi na kuwajengea mazingira stahiki ya kazi pamoja na mafao.
Serikali nitakayoongoza itaunda Tume Maalum ya Kupendekeza mishahara ya watumishi Serikalini, sekta ya umma na binafsi kwa maana ya kima cha chini cha mshahara.
Kumi na tano, tutaimarisha Muungano wetu ikiwa ni pamoja na umoja, usalama na udugu wa Watanzania kwa misingi ya haki na usawa.
Kumi na sita, tutaimarisha uhusiano na kuongoza ushirikiano na nchi nyingine ndani ya Jumuia ya Afrika ya Mashariki, SADC, Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Taasisi nyingine za Kimataifa.

0 comments:

 
Top