Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli ametoa muda kwa wala rushwa nchini kutubu dhambi zao kabla hajawa rais na watakaofanya hivyo alishawasamehe saba mara sabini lakini baada ya hapo akiingia Ikulu “atalala nao mbele”. 

Dk Magufuli ambaye juzi alitamka kuwa atawafunga kwa makufuli mafisadi wote akiingia Ikulu, jana akiwa Kongwa mkoani Dodoma alisema kitendo cha baadhi ya watu kuendelea kula rushwa na kuwanyonya watu wa hali ya chini kinamkera na hayuko tayari kuendelea kuona hali hiyo ikiendelea. 

Akihutubia mkutano wa hadhara katika mji mdogo wa Kibaigwa wilayani Kongwa, mgombea huyo alisema ndani ya Serikali kuna watu wachache ambao wanaendelea kutokuwa waaminifu na akasema hali hiyo ni kasumba na mtu wa aina hiyo hata akipewa mshahara wa Sh20 milioni kwamwezi bado atakuwa ni tatizo. 

“Mimi sikuomba urais kwa majaribio, nipeni kazi hii niwashughulikie, walarushwa wote naomba waanze kutubu mapema lakini wakichelewa hadi Oktoba 25, nitalala nao mbele na hakutakuwa na msamaha wala kumhamisha mtu kama kaharibu mahali, atabaki hapo akiwa hana kazi,” alisema. 

Akizungumzia kero kubwa ya Wilaya ya Kongwa, alisema amechoka kuzika watu wasiokuwa na hatia, hivyo akiwa rais atahakikisha viongozi wote wanawajibika na wasipofanya hivyo atawafukuza. 

Dk Magufuli alikuwa akizungumzia mgogoro wa ardhi baina ya wakulima na wafugaji wilayani Kiteto ambako watu kadhaa wamekwishauawa. 

Alisema wakuu wa mikoa, wilaya, makamanda wa polisi na maofisa tarafa katika maeneo husika wanatakiwa kukaa mguu sawa kwani siku yakitokea mauaji kwenye maeneo yao, basi watatakiwa kuachia ngazi. 


Alieleza kushangazwa kwake na mauaji hayo kuwa ya upande mmoja zaidi hasa kwa wakulima na kusema muda umefika kama wakulima wataendelea kuuawa basi ng’ombe za waliosababisha vifo hivyo wataliwa kwenye misiba. “Wakulima nataka mlime sana hata usiku limeni tu na nyinyi wafugaji nataka mfuge kwa bidii na kama maeneo hayatoshi basi mtambue kuwa rais ndiye mwenye mamlaka ya kutoa ardhi na kutenga kwa matumizi mengine ili muweze kunufaika, nitafanya hivyo,” alisema. 

Aliwataka wanachama wa Chadema kumpa kura za kutosha ili awasaidie wananchi wa Kibaigwa kuondoa kero za ushuru mdogo mdogo pamoja na kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi ili maisha ya Watanzania yabadilike. Ahadi nyingine aliyotoa ni kusimamia mikataba kwa madereva wa magari na matreka ili nao waboreshe maisha yao ikiwamo pensheni kwa wastaafu kwa kuwa waliitumikia nchi kwa uadilifu. Akiwa wilayani Mpwapwa, aliahidi mambo mawili makubwa ikiwamo ujenzi wa barabara ya lami kutoka Chipogolo kupitia Gulwe hadi Mbande na kurudisha chuo cha utafiti wa mifugo ambacho ni cha muda mrefu lakini siku za hivi karibuni kilitangazwa kuhamishiwa mjini Dodoma.

 Mgongano CDA Akiwa mjini Dodoma, Dk Magufuli alisema atashughulikia mgongano wa masilahi ambao umekuwapo kati ya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na manispaa. Alisema CDA imekuwa hailipi fidia inayostahili kutokana na sheria na kwamba endapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi, atapiga marufuku mamlaka hiyo kuchukua ardhi ya mtu yoyote bila kulipa fidia inayostahili. Alisema endapo atapata nafasi hiyo, atajenga viwanda kulingana uzalishaji wa mazao kwenye eneo husika. 

Amtetea aliyehama Chadema Katika tukio jingine, Dk Magufuli alimtaka Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, David Misime kuwashughulikia watu wote wanaomtumia ujumbe wa vitisho aliyekuwa meneja kampeni wa mgombea ubunge kwa tiketi ya Chadema Dodoma Mjini, Khalid Zoya aliyejiunga na CCM. 

Alitoa agizo hilo jana wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Jamhuri. “Ameniambia kuwa ameanza kupokea ‘meseji’ za vitisho… Najua RPC una utaalamu wa kushughulika na hili na bahati nzuri wewe ni mtendaji mzuri,” alisema Dk Magufuli huku akisogea kwa Misime. 

Akizungumza katika mkutano huo, Zoya aliahidi kuzunguka katika kata zote za Jimbo la Dodoma Mjini kuhakikisha kuwa Dk Magufuli na mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Anthony Mavunde wanachaguliwa. Akizungumzia kuhama kwa Zoya, Mwenyekiti wa Chadema mkoani Dodoma, Jella Mambo alisema: “Si jambo geni kuhamahama vyama, alikuwa CCM akaja Chadema sasa amerudi CCM tunamtakia kila la kheri.”

0 comments:

 
Top