Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha wananchi CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad  amesema kuwa, hakuna malalamiko yoyote yaliyowasilishwa siku ya kupiga kura visiwani humo.

 Maalim Seif ameyasema hayo leo kufuatia kuwepo kwa taarifa kuwa, maafisa wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imewaita mawakala wa chama tawala CCM, katika kiwanda cha Makonyo Wilaya ya Chake Chake, ili kujaza fomu za malalamiko zitakazotumika katika kudai kuwa, zilikuwepo kasoro kadhaa katika zoezi hilo. 

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Chama hicho zilizoko eneo la Mtendeni Mjini Zanzibar, Maalim Seif amesema kuwa, njama hizo za CCM wameshazigundua na kwamba hawatozikubali. Amesisitiza kuwa, njia pekee ya kuondoa utata kuhusiana na uchaguzi huo ni kukamilisha uhakiki wa majumuisho na kutangaza matokeo ya uchaguzi huo.


 Aidha ameongeza kuwa, yeye na chama chake, wataendeleza juhudi za kulipatia ufumbuzi suala hilo kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa ili kutangazwa mshindi wa Urais kufikia tarehe Pili Novemba mwaka huu. Wakati huo huo msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania Jaji Francis Mutungi amesema kuwa, upo umuhimu mkubwa kwa viongozi wa vyama vya siasa visiwani Zanzibar kukutana pamoja kwa lengo la kutatua mzozo wa kisiasa uliojitokeza.

 Mutungi amesema kwamba, Zanzibar ni mahala pa amani, hivyo hakuna haja ya kuruhusu migogoro ya aina hiyo ambayo inaweza kupelekea kuvurugika kwa amani hiyo na kuipotezea sifa yake katika jamii ya Kimataifa. 

Akiambatana na baadhi ya wajumbe wa ofisi hiyo ya msajili pamoja na msajili wa vyama kwa upande wa Zanzibar Bw. Rajab Baraka, ametoa ushauri huo wakati akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, nyumbani kwake Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar. 

Amesema kuna kila sababu ya kulinusuru taifa kuingia katika migogoro isiyokuwa ya lazima, na kutaka juhudi za makusudi zichukuliwe ili kumaliza mgogoro huo.
Chanzo radio tehran

0 comments:

 
Top