MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu amesema Rais Jakaya Kikwete anapaswa kutangaza msimamo wake iwapo yuko tayari kukabidhi serikali kwa wapinzani iwapo watashinda uchaguzi mkuu Oktoba 25 mwaka huu.
Lissu ametoa kauli hiyo jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, Jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam, mbele ya mgombea urais anayewakilisha UKAWA, Edward Lowassa.
UKAWA ni Umoja wa Katiba ya Wananchi ulioundwa na vyama vinne ambavyo ni Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD).
Lissu amesema iwapo Rais Kikwete hatatoa msimamo kuhusu utayari wa kukabidhi serikali kupisha UKAWA, wao watampeleka Lowassa Ikulu kwa nguvu ya umma.
“Mabadiliko ni pamoja na Katiba mpya, jambo la kwanza kulifanya iwapo tutaandika Katiba mpya, tumemuomba Rais Kikwete atueleze utaratibu wa kukabidhi serikali ukoje na asisingizie kuwa halipo kwenye Katiba.
“… Na kama (CCM) hawapo tayari kukabidhi madaraka sisi tutampeleka Lowassa Ikulu kwa nguvu ya Umma,” amesema Lissu ambaye naye anagombea ubunge jimbo la Singida Mashariki mkoani Singida.
Mgombea ubunge jimbo la Kawe ambaye anawakilisha UKAWA kupitia Chadema, Halima Mdee, amesema “Tuwaambie Tume ya Taifa ya Uchaguzi tunataka madaftari ya walioandikishwa kupiga kura kwenye kila kituo kilichotumika kuandikisha wananchi.”
“Mamilioni ya Watanzania hawana uhakika kama siku ya kupiga kura majina yao yatakuwepo. Tunajua CCM wameandaa kadi feki nyingi sana za kupigia kura. NEC wasipofanya hivyo tutaandamana mdogomdogo hadi Ikulu,” amesema Mdee.
Mdee ambaye anatetea kiti hicho alichoingia baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010, aliombewa kura na Lowassa akimsifia kuwa ni mbunge mchapa kazi hodari.
Mwenyekiti wa muda wa CUF, Twaha Taslima ambaye pia ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, amesema ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliomfanya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuridhia kuanzishwa vyama vya upinzani nchini.
Taslima ambaye kitaaluma ni mwanasheria na wakili katika Mahakama Kuu, amesisitiza kuwa bila ya upinzani imara nje ya CCM, chama hicho kitaendelea kutawala milele na ubovu wake.
“Nilitumaini kuwa tunaweza kupata chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuongoza nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama Cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake,” amesema wakili Taslima akinukuuu maandishi ya Mwalimu Nyerere katika kitabu cha alichokiita “Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania” ukurasa wa 66.
Mgombea Ubunge wa CHADEMA awatisha polisi
Friday, October 02, 2015
MGOMBEA ubunge jimbo la Dodoma Mjini kupitia Chadema, Benson Kigaila amelitaka jeshi la polisi kufanya shughuli za kwa kufuata misingi ya kisheria na wasikubali kutumiwa na wanasiasa.
Mbali na hilo amesema iwapo jeshi la polisi litashindwa kufanya kazi zao basi watangaze wazi kuwa ni jeshi la kisiasa na siyo vinginevyo.
Kigaila alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wana habari juu ya mwenendo wa kisiasa kwa kudai kwamba jeshi la polisi mkoa wa Dodoma linawaonea wanachama wa vyama vya UKAWA na kuwabeba wagombea wa CCM.
Amesema inasikitisha kuona jeshi la polisi linafanya kazi za kisiasa badala ya kufanya kazi kwa kuzingatia haki na usawa.
“Tumeshuhudia jinsi jeshi la polisi linavyowabeba wagombea wa CCM kwa kuwapatia ulinzi lakini sisi tumekuwa hatupewi ulinzi na matokeo yake wanadai tunafanya fujo.
“Mbaya zaidi tunasikitishwa na jeshi la polisi kuanza kuwakamata vijana kwa madai kwamba ni wazurulaji hivyo ni vitisho kwa vijana na wanatumiwa na viongozi wa CCM,” amesema Kigaila.
Mgombea huyo amesema kwamba kwa sasa Chadema inakabiliana na upinzani wa vyama viwili ambavyo alivitaka kuwa ni CCM na jeshi la polisi ambalo linafanya kazi ya siasa.
Hata hivyo Kigaila alilitaka jeshi la polisi kutoingilia mambo ya kisiasa kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha machafuko.
“Tunajua kazi ya jeshi la polisi hivyo ni vyema wakaiweka mbali na siasa ila watimize wajibu wa kwa mujibu wa sheria taratibu na kanuni na kama wataendelea kutumiwa na CCM kama wanavyofanya hatutakubali,” amesema Kigaila.
Kwa upande wake mkuu wa polisi mkoa wa Dodoma, David Misime amesema jeshi la polisi halifungamani na chama chochote cha siasa na litakabiliana na mtu yoyote bila kujali cheo wala chama