TAARIFA KUHUSU USHIRIKI WA DK. WILBROD SLAA KATIKA KAMPENI ZA
CHAMA  cha ACT-Wazalendo kimekuwa na mawasiliano na Dk. Wilbrod Peter Slaa, mwanasiasa nguli wa upinzani nchini, kuhusu uwezekano wa yeye kushiriki katika kampeni za Chama chetu kwa lengo la kuendeleza vita  dhidi ya ufisadi nchini.


Tunamshukuru sana Dk. Slaa kwa imani aliyo nayo juu ya chama chetu na uamuzi wake wa kuikabidhi  rasmi ACT-Wazalendo, mikoba yake ya vita dhidi ya ufisadi nchini.

Dk. Slaa anaamini kwamba chama chetu cha ACT-Wazalendo ndicho chama pekee chenye uhalali na uwezo wa kupambana na ufisadi baada ya chama chake cha zamani kuitelekeza vita hiyo. Dk. Slaa alikuwa ashiriki kikamilifu katika kampeni za uchaguzi zinazoendelea kupitia jukwaa la ACT-Wazalendo.

 Alikuwa aanze na Mkutano wa hadhara Mjini Iringa siku ya Jumatano tarehe 7 Oktoba 2015, na baadaye angeendelea na mikutano mingine katika majimbo mbalimbali na kuhitimisha kampeni hizo katika Viwanja vya Mwembeyanga Jijini Dar es Salaam, ambao ndio uwanja ambapo vita dhidi ya ufisadi ilitangazwa rasmi mnamo tarehe 15 Septemba 2007.

Baada ya tathmini ya kina chama cha ACT-Wazalendo kimejiridhisha kwamba hali ya usalama wa Dkt Slaa ni ndogo sana kwa sasa kutokana na vitisho mbalimbali anavyovipata. Kutokana na hali hiyo ya vitisho dhidi ya usalama wake, chama chetu kimejiridhisha kuwa hakina uwezo wa kumhakikishia Dk. Slaa usalama wake atakapokuwa majukwaani.

Kwa kuzingatia maelezo ya hapo juu, chama chetu kimefuta mikutano yote ambayo Dk. Slaa alikuwa aifanye kupitia jukwaa la ACT-Wazalendo. Chama kitaendelea kutambua mchango wake katika harakati za kukuza demokrasia na hasa bidii yake ya kujitoa katika kupambana na ufisadi nchini. Tunamuahidi kwamba chama chetu kitaendeleza vita hii kwa bidii kubwa na juhudi zake kamwe hazitapotea.

 Tunamtakia Dk. Slaa na familia yake maisha mema.

Samson Mwigamba
    KATIBU MKUU

0 comments:

 
Top