Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ametoa mwito wa kufanyiwa mabadiliko muundo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kukifanya chombo hicho kuwa taasisi shirikishi yenye kujumuisha nchi za pembe mbalimbali za dunia. Kiongozi huyo ametoa mwito huo wakati alipohutubia kikao cha 70 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.
Kwenye hotuba yake, Rais Zuma ametaja mambo mengi muhimu yanayoashiria umuhimu wa kufanyiwa marekebisho Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Kiongozi huyo mbali na kutaja mapungufu ya baraza hilo, amesema katika kipindi cha miaka 70 iliyopita, Umoja wa Mataifa pamoja na baraza lake la usalama umeweza kufikia malengo mengi muhimu na kubadilisha hali ya mambo duniani kwa kiwango kikubwa.
Wito wa kutaka yafanyike mabadiliko kwenye muundo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ulianza kutolewa tangu muongo wa 90. Mwaka 2005 viongozi wa dunia walitoa pendekezo la pamoja la kubadilishwa taasisi hiyo lakini hadi hivi sasa pendekezo hilo halijafanyiwa kazi kutokana na kukosekana irada thabiti ya kisiasa kutoka kwa nchi 5 ambazo ni wanachama wa kudumu baraza hilo.
Rais wa Afrika Kusini amesema tangu mwaka 1945 baada ya vita vya pili vya dunia, mambo mengi yamebadilika. Amesema, baadhi ya nchi zilizokuwa na nguvu na uwezo mkubwa wa kijeshi na kiuchumi kwa sasa zimeporomoka na mahapa pao pamechukuliwa na nchi ambazo wakati huo zilikuwa dhaifu kijeshi, kisiasa na kiuchumi. Kwa mfano amekumbusha kuwa nchi nyingi za Afrika wakati huo zilikuwa chini ya ukoloni lakini kwa sasa nchi zote za bara hilo ziko huru na baadhi yake zina nguvu na satua kubwa ndani ya bara hilo na kimataifa. Ni kutokana na ukweli huo ndio maana Rais Zuma akasema mabadiliko hayo yanapaswa kuwa sababu tosha ya kuchochea madadiliko kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Bara la Afrika limekuwa likitaka kupewa japo viti viwili vya kudumu kwenye baraza hilo lenye jukumu la kuchukua maamuzi muhimu kwa niaba ya dunia. Rais Zuma amesema, bara la Afrika lina idadi kubwa ya watu ikilinganishwa na bara Ulaya na kwa mantiki hiyo haoni ni kwa nini Ulaya iwe na viti vitatu vya kudumu kwenye Baraza la Usalama ilihali Afrika haina kiti hata moja. Ulaya inawakilishwa na Uingereza, Ufaransa na Russia. Wanachama wengine wa kudumu wa Baraza la Usalama ni Marekani na China.
Tayari Kansela wa Ujerumani, Angela Markel amesema anaunga mkono juhudi za Afrika za kutafuta viti viwili vya kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Nataifa. Merkel amesema kuwa, mabadiliko muhimu kwenye Baraza la Usalama ni jambo linalozungumziwa na mataifa mengi na kwamba utendaji wa hivi sasa wa baraza hilo hauzifurahishi nchi nyingi.
Katika miaka ya hivi karibuni, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeachana kabisa na malengo yake ya asili ya kusimamia amani na usalama duniani na badala yake limekuwa ni chombo cha kutunishiana misuli nchi wanachama hususan kati ya kambi ya Mashariki inayojumuisha China na Russia kwa upande mmoja na kambi ya Magharibi inayozijumuisha Marekani, Uingereza na Ufaransa kwa upande wa pili.
0 comments:
Post a Comment