Mtazamo chanya wa viongozi wa Mali kwa mazungumzo na wapinzani
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Mali amesema kuwa, serikali ya nchi hiyo ina matumaini ya kufikia mwafaka na wapinzani na hivyo amani na utulivu kushuhudiwa tena nchini humo. 

Abdoulaye Diop amesema kuwa, ana matumaini ya kupatikana natija nzuri katika mazungumzo yanayoendelea nchini Algeria kati ya ujumbe wa serikali ya Mali na makundi ya upinzani.

Duru ya tatu ya mazungumzo ya amani kati ya ujumbe wa serikali ya Bamako na wapinzani ilianza Jumanne ya tarehe 21 Oktoba huko Algiers mji mkuu wa Algeria. 

Duru za karibu na serikali ya Mali zinasema kuwa, viongozi wa Bamako wanasisitiza kwamba, kuheshimiwa mamlaka ya kitaifa, umoja na mshikamno wa wananchi pamoja na kuhifadhiwa mfumo wa Jamhuri ni mistari myekundu katika mazungumzo hayo. Duru ya pili ya mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Mali na makundi ya wapinzani ya kaskazini mwa Mali ilifanyika nchini Algeria mwanzoni mwa Septemba. 

Aidha duru ya kwanza ya mazungumzo hayo ilimalizika tarehe 20 Julai kwa kutiwa saini ramani ya njia. Kuainishwa fremu ya mazungumzo ya amani na kupatikana njia ya utatuzi jumla kuhusiana na mgogoro wa Mali ndiyo yaliyokuwa matunda ya duru mbili zilizopita za mazungumzo hayo. 

Sambamba na kuanza duru mpya ya mazungumzo hayo, David Gressly mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Mali amesema kuwa, mazingira yanayotawala hivi sasa katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ni mabaya.

 Modibo Keita Waziri Mkuu wa zamani wa Mali ambaye anashiriki katika mazungumzo ya amani na wapinzani akiwa mwakilishi wa Rais amesisitiza kwamba, katika duru hii ya mazungumzo pande mbili zitazama zaidi katika masuala yanayozusha hitilafu na kubainisha kwamba, ana matumaini duru hii ya mazungumzo itamalizika kwa pande husika kutiliana saini.

 Harakati ya Taifa ya Ukombozi wa Azawad (MNLA), Baraza Kuu kwa Ajili ya Umoja wa Azawad (GCUA) na Harakati ya Kiarabu ya Azawad (MAA) ni miongoni mwa makundi yanayoshiriki katika duru ya mara hii ya mazungumzo ya amani nchini Algeria.

Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, licha ya makundi sita ya upinzani kushiriki katika mazungumzo ya amani ya mara hii nchini Algeria, lakini kutoshiriki makundi yenye misimamo mikali kama Ansarudeen na Harakati ya Tawhidi na Jihad Magharibi mwa Afrika ni jambo linalotilia shaka juu ya kupatikana amani ya kudumu katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. 

Baadhi ya weledi wa mambo wanaamini kwamba, kupatikana amani ya kudumu kaskazini mwa Mali kunakinzana wazi na matakwa na stratejia ya Ufaransa ambayo ni kudhibiti vyanzo vya utajiri vya eneo hilo magharibi mwa Afrika.

 Lakini pamoja na hayo, viongozi wa serikali ya Mali wana matumaini makubwa na duru hii ya mazungumzo na wanayatazama mazungumzo ya mara hii kwa mtazamo chanya. 

Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Mali akasema kuwa, ana matumaini mara hii mazungumzo hayo yatakuwa na matunda maridhawa na hivyo kuifanya nchi hiyo ishuhudie tena amani na uthabiti.

chanzo Radio tehran

0 comments:

 
Top