Tunda hili linasaidia uyeyushaji wa chakula tumboni hasa kwa wale wenye matatizo ya vidonda tumbo, kwani lina ufumwele ambao ni muhimu katika kukinga kuta za utumbo.

Tunda hili ni lenye faida nyingi kiasi kwamba baadhi ya watu wamelipa jina la malkia wa matunda. Kuna ambao wamethubutu kuliita parachini kuwa ni aina nyingine ya ndizi na ingawa huko nyuma tunda hilo halikuzingatiwa sana lakini kutokana na faida zake nyingi kiafya na pia katika masuala ya vipodozi, hivi sasa avocado ni  miongoni mwa matunda yanayosifika sana duniani. Tunda hili lina kiasi kidogo cha maji tofauti na matunda mengi tuliyozea kula, lina kiwango kikubwa cha mafuta na ndani yake pia kuna tindikali (acid) aina mbalimbali zinazosaidia kukinga na kutibu maradhi mwilini. Parachichi pia lina kiwango cha juu cha protini na pia vitamin E. Inaelezwa kuwa, vitamin E iliyoko wenye avocado ni nyingi zaidi kuliko ile inayopatikana kwenye vyanzo vya wanyama, na kwamba hata mayai hayana kiwango kikubwa cha protein ikilinganishwa na avocado. Sifa hiyo inalifana parachichi kuwa tunda linalopendwa sana kuliwa na wanamichezo hasa wale wanaopenda kujenga miili yao kwa kutumia amino acids. Virutubisho vingine vinavyopatikana kwenye avocado ni vitamin B6, madini ya chuma na madini ya potassium.
Tunda la avocado ni chakula kizuri kwa watoto hasa kutokana na ulaini wake, na virutubisho lilivyonavyo vinaweza kuwapa nafuu wale wenye matatizo ya mfadhaiko na matatizo ya uzazi kama ugumba na utasa. Tindikali aina ya oleic iliyomo ndani ya parachichi inasaidia kukinga magonjwa ya moyo, kiharusi na kansa. Aidha tunda hili linasaidia uyeyushaji wa chakula tumboni hasa kwa wale wenye matatizo ya vidonda tumbo, kwani lina ufumwele ambao ni muhimu katika kukinga kuta za utumbo. Wale wenye kusumbuliwa na ukosefu wa damu, kisukari, matatizo ya mfumo wa neva na mishipa ya damu wanashauriwa kula avocado mara kwa mara. Pia tunda hili limethibitishwa kupunguza kiwango kikubwa cha mafuta mabaya ya cholesterol kwenye damu hasa kwa watu  ambao ni wanene

Wataalamu wa dawa asilia wanatujuza kuwa, majani ya mti wa avocado pamoja na magamba ya mti wake yakitengenezwa vizuri yanatumika kutibu maradhi ya kuharisha, kuondoa gesi tumboni, kutuliza kikohozi pamoja na matatizo ya ini na kusafisha njia ya mkojo. Dawa hii haishauriwi kutumiwa na akina mama wajawazito kwani inaweza kuwasababishia matatizo yanayoweza kuharibu mimba. Aidha kwa wanawake ambao wameshindwa kuona siku zao kwa wakati, wanaweza kutumia mchanganyiko huo kutatua tatizo hilo.

Ama kwa matumizi ya nje ya mwili parachichi husaidia kulainisha ngozi na kuondoa makunyanzi, kung'arisha na kulainisha nywele na kuzifanya zionekane nadhifu, pia linasaidia ukuaji wa nywele, kuziimarisha na kuzizuia kukatika.

0 comments:

 
Top