Mr., kibindo
TATIZO SI MADARAJA YA UFAULU

Sekta ya elimu nchini imejikuta kwenye wakati mgumu wa kudhoofika kwa hali ya elimu nchini licha ya  ongezeko kubwa la shule na vyuo vya elimu ukilinganisha na kipindi cha uhuru miaka ya 1961 ambapo shule zilikuwa chache lakini ufaulu ulikuwa mzuri ukilinganisha na ilivyo sasa.

Kufuatia hali hii sekta ya elimu imejaribu kuja na mikakati tofauti ya kutatua tatizo hili katika makala hii tutatazama mkakati uliozua maswali mengi uliotambulika kwa lugha ya wenzetu kama “THE BIG RESULT NOW”yaani matokeo makubwa sasa.

Mkakati huo umelenga kuongeza hali ufaulu kwa wanafunzi.Sina lengo la kuupinga moja kwa moja mkakati huu kwa kuwa vipo vipengere muhimu kwa mtazamo wangu mfano matumizi ya alama endelevu ambayo yatamsaidia manafunzi kupata alama anazostahili katika matokeo ya mwisho.

Huwa Napata shaka kama waliopewa dhamana ya kusimamia elimu hawafahamu chanzo halisi cha matokeo mabaya au ndiyo siasa imewatawala?nisielekee huko sana ila mantiki yangu hapa ni kujaribu kueleza matatizo yanayoitafuna sekta hii nyeti kwa kupitia mitazamo mbalimbali ya wasomi pamoja na wadau wengine wa elimu.

Kwa kuanzia Mnamo tarehe 26 Novemba mwaka 2011 shirika la HakiElimu kwa kushirikiana na Umoja wa walimu wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSTA)waliandaa kongamano lenye lengo la kutathmini hali ya elimu nchini; miaka 50 tangu Tanzania Bara kupata uhuru wake mwaka 1961.

Kongamano hilo liliithibitisha kwa takwimu ongezeko la idadi ya shule na vyuo, idadi ya uandikishwaji na usawa baina ya wanafunzi wa kike na kiume. Kwa mfano lilisifu mafanikio katika ongezeko la idadi ya shule za msingi kutoka shule 338 tu mwaka 1961 hadi zaidi ya 15,000. Pia lilisifu ongezeko la idadi ya shule za sekondari kutoka 41 tu mwaka 1961 tu mwaka 1961 hadi 4,367 mwaka 2011.

Hata hivyo pamoja na mafanikio hayo zilibainika changamoto mbalimbali ambazo zinaikabili sekta ya elimu changamoto hizo ni pamoja na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaoshindwa  mitihani, na kuporomoka kwa ubora wa elimu. Mfano uwepo wa watoto wanaohitimu darasa la saba bila kujua kusoma na kuandika.

 Aidha, kumekuwa na uhaba mkubwa wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia pamoja na ukosefu wa waalimu bora ambao ni muhimu kwa utoaji wa elimu bora.

Changamoto nyingine ni maslahi mabovu ya walimu na watumishi wa ngazi za kawaida mashuleni.

Aliyewahi kuwa Waziri wa Elimu katika serikali ya kwanza, Jackson Makwetta alisema kuporomoka kwa elimu nchini kunatokana na Tanzania kuwa na viongozi wababaishaji, wasemaji wa maneno mengi, wasiotekeleza wanayoyasema na kukosa ufuatiliaji.

Naye Dk. Kitila Mkumbo alisema kuwa, kwa sasa taifa lazima liamue kukubaliana na maoni ya wataalamu kuhusu lugha ya kufundishia kama iwe ni Kiswahili, hali aliyosema itawasaidia wanafunzi kuelewa vyema wanachofundishwa darasani.

Kama sivyo basi Kiingereza kifundishwe vizuri ili wanafunzi wakielewe na waweze kukitumia ipasavyo.

Kinachosisistizwa na watoa mada na washiriki wa Kongamano hili ni kuwa, pamoja na kwamba tunastahili kujivunia mafanikio tuliyofikia tangu uhuru lakini tufikie mahala wanapata elimu bora ili waweze kukabiliana na changamoto zinazowazunguka pamoja na jamii zao.

Imefika wakati  badala ya kuendelea kujenga shule mpya, pengine sasa tuangalie zaidi namna ya kuboresha ufundishaji na ufundishwaji katika zile shule zilizopo ili wanafunzi wapate ujuzi wanaohitaji sasa na baadaye katika maisha yao.

Ujuzi au uwezo huu ni pamoja na ule utakaomuwezesha mwanafunzi kujiamini na kujituma, kuweza kutatua matatizo na kukabiliana na changamoto kwa ufanisi na kuchambua na kutathmini taarifa kwa ufasaha na umakini zaidi.

Elimu yetu inapaswa iwape wanafunzi uwezo wa kutumia mitazamo waliyojifunza kwenye eneo moja katika maeneo mengine pamoja na kuwapa  uwezo wa kuelewa na kuwa tayari kuchangia mahitaji ya jamii zao na taifa kwa ujumla.

Dk. Hillary Dachi yeye alizungumzia zaidi kuporomoka kwa hadhi ya ualimu tangu nchi ilipopata uhuru kiasi kwamba sasa hivi walimu wanaishi maisha ya dhiki na wengi hawaipendi kazi hiyo.

Dk. Dachi anaona kuwa taifa halitapata waalimu wa kutosha ikiwa hakuna juhudi za makusudi za kumfanya mwalimu aliyepo aendelee kufanya kazi yake kwani kwa sasa wengi hukimbia taaluma zao za ualimu na kuhamia katika taaluma zingine.

 Walimu wamekata tamaa; uwajibikaji umepungua; na uwajibikaji umepungua kwa wananchi. Kwa wazazi, tunajiona kwamba wajibu wetu ni kuwapeleka watoto shuleni na kuchangia tu na si kufuatilia matokeo yao.

Kukosekana kwa Bodi ya taaluma ya ualimu ambayo ingeweza kusajili walimu na kusimamia maadili na mambo mengine yanayohusiana na taaluma ya ualimu. Hatuna vyama vya kitaaluma vya walimu. Mfano zamani kilikuwepo chama kinaitwa Chama cha Kitaalamu cha Walimu Tanzania yaani (CHAKWATA)

Ualimu umepoteza hadhi na heshima yake katika jamii. Ni kazi ambayo kwa vijana wengi ni chaguo lao la mwisho.Mfano imezoeleka sana nchini kwa mtoto asipo-fanya vizuri. Kwa maneno mengine akifeli akapata madaraja ya chini sana tunasema mtafutie angalau kozi ya ualimu.

Wakimkuta pale nyumbani ukasema bado nahangaika unajua hakufanya vizuri wanasema ina maana umekosa hata kozi ya ualimu? Hata ualimu umekushinda? Hali hii inasikitisha sana.

Walio wengi, taaluma ya ualimu ni kama suluhisho la maisha kwamba unapokosa kila kitu, anakuwa hana jinsi ila ni kukimbilia kujifunza ualimu.

Na kwa sababu ukiwa katika ualimu ni rahisi sana kujiendeleza, kwa hiyo walio wengi wanabadilisha taaluma wanaenda katika taaluma nyingine.  

Hali hii inasababisha ugumu wa kupata walimu wa kutosheleza kwa sababu hakuna namna yeyote tunayoifanya kama serikali kuhakiki-sha kwamba walimu wanaipenda kazi yao, wanaendelea kufundisha na wanapenda kufahamika kama walimu.

Ifike mahala sasa serikali ifanyie kazi changamoto hizi badala ya kuhangaika kubadilisha madaraja wakizani kuwa ndiyo suluhisho la kuporomoka kwa ubora wa elimu Tanzania.

Yapo mengi ya kueleza ila haya niliyoeleza yanatosha kuwa kianzio tosha kwa waliopewa dhamana ya kusimamia elimu nchini,wadau wa elimu na watanzania kwa ujumla kushikamana na kila mmoja kuwajibika katika nafasi yake ili kuinusuru elimu yetu kwa mustakabali wa vizazi vyetu naTaifa kwa ujumla.

By


Undergraduate at Tumaini University Dar es salaam.

0 comments:

 
Top