Rais Magufuli Ampa Pole Tundu Lissu kwa Kupigwa Risasi


Rais John Magufuli, amesema amepokea kwa masikitiko tukio la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Katika akaunti yake ya Twitter, Rais Magufuli amesema anamuombea Lissu kwa Mwenyezi Mungu aweze kupona haraka.

“Aidha, vyombo vya dola viwasake wale wote waliohusika na tukio hili la kinyama na kuwafikisha ktk mikono ya sheria,” amesema.

Lissu amejeruhiwa leo Alhamisi mchana akiwa kwenye gari nyumbani kwake Area D na sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.



CCM Yatoa Tamko Tundu Lissu Kupigwa Risasi

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole kimelaani kitendo alichofanyiwa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu kwa kupigwa risasi leo mchana nyumbani kwake Dodoma.

Taarifa hiyo ya CCM inalaani kitendo hicho cha kikatili na kusema si kitendo cha utu hivyo kimelitaka jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kuwachukulia sheria kali wote ambao watapatikana kuhusika katika tukio hilo. 

Chadema yatoa tamko Tundu Lissu kupigwa risasi

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimepokea kwa mshtuko taarifa ya kupigwa risasi mwanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu.

Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki, amepigwa risasi baada ya kikao cha Bunge mchana wa leo Alhamisi.

Shambulio hilo limetokea leo mchana nyumbani kwa Lissu, Area D mjini Dodoma na sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

“Chadema tunalaani vikali kitendo hicho na tunafuatilia kwa karibu hali yake,” imesema taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Uenezi, Mawasiliano na Mahusiano ya Nje ya Chadema makao makuu.

Wakati huohuo, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umesema umepokea kwa mshtuko taarifa za kupigwa risasi Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS).

Mratibu wa mtandao huo,  Onesmo ole Ngurumwa katika taarifa amesema wanatoa pole kwa familia ya Lissu, wananchi wa Singida Mashariki, wanachama wa TLS na Watanzania kwa jumla.

Mtandao huo umewahimiza Watanzania wote kumwombea Lissu.

Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge, Job Ndugai amewasili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambako Lissu anaendelea na matibabu.                       

Pia, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amefika hospitalini hapo ambako Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, James Charles amesema Lissu yu hai na imara.

Dk Charles akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi uliopita amesema mbunge huyo amepigwa risasi tumboni na kwamba timu ya madaktari inaendelea na matibabu.


Polisi Wazungumzia Tukio la Tundu Lissu Kupigwa Risasi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amezungumzia tukio la kupigwa risasi mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, akiwaomba wananchi wenye taarifa kulisaidia jeshi hilo.

Muroto amesema leo Alhamisi kuwa wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na wameshafika eneo la tukio nyumbani kwa Lissu.

“Tunaomba mwananchi wenye taarifa atusaidie. Jeshi la Polisi tumeanza uchunguzi, tumefika eneo la tukio na tunaendelea,” amesema.

Kamanda Muroto amesema taarifa za awali zinaonyesha kuna gari aina ya Nissan lenye rangi nyeupe lilikuwa likimfuatilia Lissu.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana amewataka wananchi kuwa watulivu wakisubiri taarifa za Jeshi la Polisi na madaktari wanaoendelea na matibabu ya mbunge huyo, ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chadema.

Akizungumza maendeleo ya matibabu ya mwanasiasa huyo ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma James Charles amesema Lissu yu hai na imara.

Amsema mbunge huyo amepigwa risasi tumboni na kwamba timu ya madaktari inaendelea na matibabu.

“Tumempokea Lissu mchana, kanuni za matibabu haziruhusu mtu mwingine asiye mtumishi kuingia chumba cha matibabu. Tuna uwezo wa kutosha wa kutoa huduma ya dharura,” amsema.

Amsema kwa sasa wanaendelea na huduma na wakikamilisha watatoa taarifa.



Mbunge wa Rombo Asimulia Jinsi Tundu Lissu Alivyopigwa Risasi

Mbunge wa Rombo, Joseph  Selasini ameeleza jinsi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alivyopigwa risasi nyumbani kwake mjini Dodoma.

Selasini amesema kuwa maelezo aliyopata ni kuwa alikuwa akifuatiliwa na  gari tangu anatoka bungeni na dereva wake alilishtukia.                      

Amesema kuwa alivyoona wanamfutilia alipofika nyumbani, dereva alimsihi Lissu asishuke ndani ya gari.                       

"Hao watu walipoona hawashuki walijifanya kuna kitu wanaangalia walivyoona kuna utulivu walisogeza gari lao ambalo ni tinted na kuanza kurusha risasi upande wa Lissu." amesema                      

Selasini amesema, “Risasi zilimpata mguuni, mkononi na tumboni lakini daktari anasema anaendelea vizuri."

Lissu amepigwa risasi leo Alhamisi  na kupelekwa chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.

Zitto Kabwe: Watanzania Tuungane Pamoja Kupinga Siasa za Mauaji

Mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini Mhe. Zitto Zuberi Kabwe amewataka wananchi kusimama imara na wasikubali kabisa kuruhusu siasa za mauji kupata nafasi nchini Tanzania.

Zitto ameeleza hayo kupitia ukurasa wake wa facebook mara baada ya kutokea taarifa ya kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Antipas Lissu na watu wasiyofahamika.

"Nchi yetu imefungua ukurasa mpya. Wananchi tusimame imara tusikubali kabisa kuingia kwenye siasa za namna hii. Mola amponye ndugu yetu", ameandika Zitto.

 Mhe. Tundu Antipas Lissu amepigwa risasi kadhaa mwilini mwake akiwa nyumbani kwake Dodoma eneo la 'area D' na watu wasiojulikana
  Ndugu lissu amepelekwa nchini Kenya kuendelea kupata matibabu.
TAFADHARI TOA MAONI YAKO HAPA

0 comments:

 
Top