Waasi wa madhehebu ya Shia wanaomshikilia nyumbani kwake Rais wa Yemen wamefikia makubaliano na kiongozi huyo anayeungwa mkono na Marekani kukomesha mzozo wa umwagaji damu katika mji mkuu. 

Gari la kijeshi lililochukuliwa na wapiganaji wa Kihouthi nje ya Ikulu ya Rais mjini Sanaa. Gari la kijeshi lililochukuliwa na wapiganaji wa Kihouthi nje ya Ikulu ya Rais mjini Sanaa.

Makubaliano hayo yaliofikiwa usiku wa manane ambayo yanawaahidi waasi kuwa na usemi mkubwa katika kuliendesha taifa hilo maskini kabisa katika ulimwengu wa Kiarabu ili waasi hao wawaondowe wapiganaji wao wanaozingira makaazi ya Rais Abed Rabbo Mansour Hadi na maeneo mengine muhimu ya mji mkuu hayakubainisha hasa nani anaongoza nchi hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Yemen SABA waasi hao wa Houthi pia wamekubali kumuachilia huru mshauri mkuu wa Hadi ambaye wamemteka nyara hivi karibuni.

Wahouthi ambao waliudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo na taasisi nyingi za serikali tokea mwezi wa Septemba wamesema walichokuwa tu wakikitaka ni mgao wa haki wa kushirikiana madaraka. 

Wahakiki wanasema wanataka kuendelea kumbakisha Hadi kama Rais kwa jina tu wakati wakishikilia hatamu za madaraka.
 
Hadi bado anashikiliwa
Wapiganaji wa Kihouthi wakiwa katika sare za kijeshi mjini Sanaa.  Wapiganaji wa Kihouthi wakiwa katika sare za kijeshi mjini Sanaa.

Baada ya mapambano ya siku kadhaa na kutekwa kwa Ikulu ya Rais wasaidizi wa Hadi wamesema amekuwa akishikiliwa nyumbani kwake baada ya waasi wa Kihouthi kuwaondowa walinzi wake na badala yake kuwaweka wapiganaji wao.

Mashahidi wanasema wapiganaji wa Kihouthi wameendelea kubakia nje ya kasri la rais na makao yake ya binafsi ambapo mkuu wa nchi ndiko anakoishi hasa .Katika taarifa yake aliyotolewa Alhamisi Rais Hadi amesema Wahouthi wamekubali kuwaondowa wapiganaji wao katika sehemu hizo.

Lakini Mohammed al - Bukhaiti mjumbe wa kamati kuu ya Wahouthi ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba kuondolewa kwa wapiganaji wao na kuachiliwa kwa mkurugenzi wa ofisi ya Hadi, Ahmed Awad bin Mubarak kutoka kizuizini kutafanyika siku mbili au tatu iwapo serikali itatekeleza masharti ya makubaliano yao.
 
Walichokubaliana
Makubaliano hayo yanamtaka Rais Hadi kuunda upya tume iliopewa majukumu ya kurasimu katiba kuhakikisha uwakilishi mzuri wa Wahouthi.Rasimu hiyo ilikuwa imependekezwa kuundwa kwa serikali ya shirikisho ya majimbo sita jambo ambalo Wahouthi wamelikataa. Makubaliano ya Jumatano yanakusudia kuundwa kwa taifa la shirikisho lakini haikutaja pendekezo la majimbo sita.

Rasi wa zamani wa Yemen Ali Abdullah Saleh. Rasi wa zamani wa Yemen Ali Abdullah Saleh.
 
Wahakiki wanamtuhumu Rais aliyepinduliwa Ali Abdallah Saleh aliyepinduliwa kutokana na uasi wa umma hapo mwaka 2011 baada ya kuwepo madarakani mwa miongo mitatu kwa kuwa na mkono wake katika njama ya Wahouthi kuudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo.

Akitaka kutumia machafuko hayo kwa faida yake Rais huyo wa zamani wa Yemen hapo Alhamisi ametowa taarifa ya nadra hadharani ambapo amemtaka Hadi kuitisha uchaguzi wa rais na bunge na mapema na kutaka kufutwa kwa vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa vilivyowekwa dhidi yake na viongozi wengine wawili wa Kihouthi hapo mwaka jana baada ya Wahouthi kunyakuwa madaraka.

Baadhi ya watu wanahofia kwamba mashambulizi hayo ya Wahouthi yanaweza kusababisha kuvunjika kwa Yemen ambayo imeungana tu hapo mwaka 1990. 

Mchambuzi wa kisiasa Mansour Hayel amesema kwamba unyakuzi wa madaraka wa Wahouthi katika mji mkuu wa nchi hiyo kunaweza kusababisha kusambaratika kwa Yemen nzima na hali inaweza kuwa mbaya sana kushinda hata ile ya Somalia.
chanzo DW

0 comments:

 
Top